UN yaonya baada ya mripuko wa kipindupindu kuua watu 20 Ethiopia
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imetoa indhari baada ya makumi ya watu kuaga dunia huku mamia ya wengine wakiathiriwa kutokana na mripuko wa ugonjwa wa kipindupindu kusini mashariki mwa Ethiopia.
OCHA imesema watu 20 wameaga dunia kufikia sasa kwa ugonjwa huo, huku kesi 491 zikinakiliwa katika mripuko wa sasa ambao unaripotiwa kuwa mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika katika miaka ya karibuni.
Taarifa ya OCHA imeeleza kuwa, mripuko wa kipindupindu umeenea katika maeneo 41 ya wilaya nne za Zoni ya Bale, katika jimbo la Oromia, na wilaya mbili za Zoni ya Liban katika jimbo la Somali.
Kwa mujibu wa ofisi hiyo ya Umoja wa Mataifa, watu zaidi ya 555,000 wapo katika hatari ya kukumbwa na kipindupindu katika wilaya sita zilizoathiriwa na mripuko wa maradhi hayo.
Takwimu za OCHA zinaonyesha kuwa, kiwango cha watu wanaokabiliwa na maradhi hayo katika wilaya za Berbere, Gura Damole, na Quarsadula kimeongezeka kwa asilimia 28 katika kipindi cha wiki mbili zilizopita.

Mashirika ya Umoja wa Mataifa, lile la Afya WHO na la Kuhudumia Watoto UNICEF, yametangaza kupiga jeki juhudi za kuzuia kuenea kwa ugonjwa huo ambayo pia inakabiliwa na mapigano katika eneo la kaskazini la Tigray.
Mwezi uliopita, Shirika la Afya Duniani lilionya kwamba baada ya miaka kadhaa ya kupungua kwa visa vya kipindupindu, lakini hivi sasa kesi za maradhi hayo zinaongezeka ulimwenguni. Kesi za maambukizi ya kipindupindu zimeripotiwa katika nchi zisizopungua 26 katika miezi tisa ya mwaka huu pekee.