Jan 09, 2023 04:09 UTC
  • Senegal yaomboleza vifo vya makumi ya watu katika ajali ya barabarani

Rais Macky Sall wa Senegal ametangaza siku 3 za maombolezo kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyosababisha vifo vya makumi ya watu mapema jana Jumapili.

Rais Sall amesema katika ujumbe aliotuma kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter kuwa, ameeleza kusikitishwa mno na ajali hiyo ya barabarani na kutangaza siku tatu za maombolezo kitaifa kuanzia leo Jumatatu.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, ajali hiyo imehusisha mabasi mawili yaliyogongana uso kwa uso katika mji wa Kaffrine, yapata kilomita 220 kusini mashariki mwa mji mkuu Dakar.

Habari zaidi zinasema kuwa, dereva wa basi moja alishindwa kulidhibiti baada ya tairi kupasuka na kupelekea kuacha njia yake na kugongana ana kwa ana na basi jingine lililokuwa likitokea upande wa pili.

Kukithiri visa vya ajali katika nchi za Afrika

Kanali Cheikh Fall, Mkuu wa Idara ya Zimamoto nchini Senegal amesema watu 38 wameaga dunia katika ajali hiyo, huku wengine 87 wakijeruhiwa. Inaarifiwa kuwa, yumkini idadi ya wahanga wa ajali hiyo ikaongezeka kutokana na majeraha mabaya waliyoyapata.

Ajali mbaya za barabarani zinatokea mara kwa mara nchini Senegal. Mara nyingi husababishwa na upakiaji kupita kiasi wa abiria, hali mbaya ya barabara, uchakavu wa vyombo vya kusafiria, ulezi na kuendesha magari kwa uzembe wa kupindukia.

Mwaka 2017, mabasi mawili yaligongana na kusababisha vifo vya watu 25 nchini Senegal, ambapo baadhi yao walikuwa wakienda katika hafla ya kidini.

Tags