Mahakama Kuu ya Malawi yamrejesha kazini mkuu wa kupambana na rushwa
(last modified Tue, 07 Feb 2023 11:48:44 GMT )
Feb 07, 2023 11:48 UTC
  • Martha Chizuma
    Martha Chizuma

Mahakama Kuu ya Malawi imeondoa zuio la serikali alilokuwa amewekewa Bi Martha Chizuma, Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa ya nchi hiyo na hivyo kutoa mwanya wa kurejea kazini.

Wiki iliyopita, Msaidizi wa Rais wa Malawi, Collen Zamba alitangaza kusimamishwa kazi kwa Bi Chizuma. Kusimamishwa kazi Martha Chizuma kulihusiana na madai aliyotoa kupitia mkanda wa sauti uliovuja ambapo alisikika akisema kuwa baadhi ya maafisa wa ngazi ya juu serikalini na baadhi ya maafisa wa mahakama wanakwamisha jitihada za kupambana na ufisadi. 

Afisa mmoja ambaye alihisi kuumizwa na matamshi ya Bi Chizuma alimfungulia mashtaka Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa ya Malawi na ndipo akasimamishwa wadhifa wake huo.

Hatua ya kumsimamisha kazi Martha Chizuma ililaaniwa na kukosolewa vikali na taasisi za kiraia, vyama vya upinzani na Chama cha Wanasheria wa Malawi. Chama hicho kilitoa taarifa kikisema kuwa mtu pekee ambaye kisheria ana mamlaka ya kumuajiri au kumfuta kazi Mkuu wa Taasisi ya Kupambana na Rushwa ni Rais wa nchi. 

Rais Lazarus Chakwera wa Malawi kwa upande wake amesema kuwa hatamfuta kazi Bi Chizuma. Aidha ametaja kurekodiwa na kusambaa kwa sauti hiyo kuwa ni jitihada za kukwamisha vita vya kupambana na rushwa.  

Rais Lazarus Chakwera wa Malawi 

Chama cha Wanasheria cha Malawi kilituma maombi ya mapitio ya hukumu ya mahakama ambayo yalikubaliwa na mahakama hiyo jana Jumatatu.