Polisi ya Nigeria yafyatua risasi Siku ya Quds na kuua mtu mmoja
Mtu mmoja ameripotiwa kuuawa na wengine wengi kujeruhiwa baada ya polisi kufyatua risasi katika maandamano ya kila mwaka ya Siku ya Kimataifa ya Al-Quds katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja na mji wa Kaduna.
Video kutoka Abuja zinaonyesha polisi wakitumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji huku washiriki wakihaha kutafuta mahali pa kujificha.
Vilevile watu walioshuhudia wamesema wamewaona polisi wakiwafyatulia risasi waandamanaji katika Siku ya Kimataifa ya Quds katika mji wa Kaduna. Hakuna majeruhi wameripotiwa.
Kabla ya kuanza kwa maandamano ya jana ya kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Quds, waandalizi walikuwa wameelezea wasiwasi wao kwamba uwepo mkubwa wa askari usalama unatishia waandamanaji.
Tume ya Kiislamu ya Haki za Binadamu ya Uingereza (IHRC) ilikuwa imeeleza wasiwasi wake kabla ya maandamano ya Abuja kuhusu uchochezi wa polisi na upotoshaji wa kimakusudi wa jeshi hilo kwamba maandamano hayo hayakuwa ya kutetea Palestina bali ni ya kuonyesha mshikamano na Sheikh Ibrahim el-Zakzaky, kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini humo.
Maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds hufanyika kila mwaka katika Ijumaa ya mwisho ya mwezi mtukufu wa Ramadhani katika miji na maeneo mengine ya Nigeria na nchi mbalimbali ili kuonesha mshikamano na watu wanaodhulumiwa wa Palestina.
Hii si mara ya kwanza kwa askari usalama wa Nigeria kuwashambulia waandamanaji katika Siku ya Kimataifa ya Al-Quds. Julai 2014, polisi wa nchi hiyo walifyatua risasi kwenye mkutano wa hadhara huko Zaria, kaskazini mwa Nigeria na kuua watu 34.
Siku ya Kimataifa ya Quds ni miongoni mwa urithi wa hayati mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Imam Ruhullah Khomeini (MA), ambaye anaenziwa kama kiongozi wa kiroho na Waislamu duniani kote. Ikumbukwe kuwa mwaka 1979, muda mfupi baada ya kuongoza Mapinduzi ya Kiislamu ambayo yalimuondoa madarakani Shah wa Iran anayekuwa akiungwa mkono na Marekani, Ayatullah Khomeini aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya mfungo wa mwezi wa Ramadhani kuwa Siku ya Quds.