Jun 18, 2023 07:33 UTC
  • Waliouawa katika mapigano ya Sudan wapindukia 3,000

Wizara ya Afya ya Sudan imetangaza kuwa, idadi ya watu waliouawa katika mapigano yanayoendelea kushuhudiwa nchini humo ni zaidi ya elfu tatu.

Haitham Muhammed İbrahim, Waziri wa Afya wa Sudan alisema hayo jana usiku na kuongeza kuwa, mapigano hayo yaliyoanza tangu Aprili 15 yamesababisha pia watu elfu sita kujeruhiwa.

Idara ya Afya jijini Khartoum iliripoti jana Jumamosi kwamba, watu 17 wakiwemo wanawake na watoto wadogo wameuawa katika shambulizi la anga katika eneo la Yarmouk, kusini mwa mji mkuu huo wa Sudan, mbali na nyumba 25 kuharibiwa.

Vita vya Sudan viliingia mwezi wa tatu Alkhamisi iliyopita, huku mashirika mbalimbali ya misaada ya kibinadamu ya kieneo na kimataifa yakitahadharisha kuhusiana na hali mbaya ya kibinadamu nchini humo na kutoa mwito wa kusitishwa vita hivyo.

Vita hivyo kati ya askari watiifu kwa Kamanda wa Jeshi la Sudan Abdel Fattah al Burhan na hasimu wake Kamanda Mohamed Hamdan Dagalo hadi sasa vimeuwa zaidi ya watu 3,000.

Kadhalika watu zaidi ya milioni 2.2 wamelazimika kuhama makazi yao huko Sudan ambapo raia zaidi ya 528,000 wamekimbilia katika nchi jirani wakihofia mapigano.

 

Tags