Pande hasimu Sudan zatakiwa kuweka silaha chini kuelekea Iddul Adh'ha
(last modified Fri, 23 Jun 2023 10:20:18 GMT )
Jun 23, 2023 10:20 UTC
  • Pande hasimu Sudan zatakiwa kuweka silaha chini kuelekea Iddul Adh'ha

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imetoa mwito kwa vikosi hasimu vinavyopigana nchini Sudan kusitisha mapigano, wakati huu ambapo taifa hilo kama mataifa mengine ya Waislamu, linakaribia kuadhimisha Sikukuu ya Iddul Adh'ha (Iddul Hajj).

Katika taarifa, Hissein Brahim Taha, Katibu Mkuu wa OIC amesema kuna haja kwa pande hasimu nchini Sudan kusitisha uhasama na kuweka silaha chini, na kufanya jitihada za kufikiwa makubaliano ya kusitisha kikamilifu mapigano hayo.

Aidha amewataka askari wanaopigana nchini Sudan kwa zaidi ya miezi miwili sasa kuyaruhusu mashirika ya kimataifa ya kibinadamu kupelekea misaada ya dharura katika maeneo yaliyoathiriwa na mgogoro huo.

Kadhalika Katibu Mkuu wa Jumuiya ya OIC amewataka wadau wote wa kieneo na kimataifa kuunga mkono jitihada za kufikiwa makubaliano na kusitisha mapigano mara moja nchini Sudan, na kuzishinikiza pande hasimu katika nchi hiyo ya Kiarabu kuheshimu mapatano hayo.

Huku hayo yakiripotiwa, pande mbili zinazopigana nchini Sudan, yaani jeshi la taifa SAF na kikosi cha msaada wa haraka (RSF) zilianza kushambuliana tena Jumatano ya juzi, baada ya muda wa kusitisha mapigano kwa saa 72 kumalizika.

Nembo ya OIC

Sudan imetumbukia katika mapigano kati ya jeshi la nchi hiyo linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan na vikosi vya msaada wa haraka RSF vinavyoongozwa na Kamanda Muhammad Hamdan Daghalo tangu Aprili 15 mwaka huu.

Mapigano hayo yanayojiri huko Khartoum na katika miji mingine ya kaskazini na magharibi mwa nchi hiyo yameua watu zaidi ya 1,000, mbali na kulazimisha mamilioni ya wengine kuyahama kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

Tags