Ulimwengu wa Michezo, Agosti 5
Karibu tuangazie japo kwa ufupi baadhi ya matukio makubwa ya michezo yaliyoshuhidiwa kote duniani ndani ya siku saba zilizopita…..
Voliboli U-18; Iran yavaana na China
Iran imeibuka mshindi wa pili kwenye Duru ya 15 ya Mashindano ya Voliboli ya Mabingwa wa Asia kwa vijana wenye chini ya miaka 18. Hii baada ya kushindwa kufurukuta mbele ya China katika mchezo wa fainali uliopigwa Jumapili katika Ukumbi wa Isa Bin Rashid huko Riffa, viungani mwa Manama, mji mkuu wa Bahrain. Hii ni mara ya kwanza kwa China kutwaa taji hilo, baada ya kuichachafya Iran seti 3-2 (23-25, 25-17, 25-19, 20-25, 15-10).
Iran ilitinga fainali baada ya kuifanyia vibaya Japan kwenye mchezo wa nusu fainali uliopigwa Jumamosi. Wairani waliwaadhibu wana Samuirai seti 3-0.
Voliboli ya Vijana: Iran bingwa wa Asia
Rais mpya wa Iran, Masoud Pezeshkian ameipongeza timu ya voliboli ya vijana wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kutwaa ubingwa wa Mashindano ya Voliboli kwa Vijana wenye chini ya miaka 20 wa Asia. Katika ujumbe wake wa tahania alioutuma kwenye mtandao wa kijamii wa X, Dakta Pezeshkian ameandika: Nautazama ushindi huu kama bishara njema katika siku za kwanza za serikali ya umoja wa kitaifa. Aidha Kiumars Hashemi, Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran ameipongeza timu hiyo ya voliboli ya mabarobaro wa Iran kwa kuibuka washindi.
Kadhalika amelishukuru benchi la ufundi, wakufunzi na maafisa wa Iran kwa kuandaa timu barabara iliyoileletea shani na heshima Iran kwa mara ya tatu mfululizo sasa. Vijana hao wa Iran wenye chini ya umri wa miaka 20 waliibuka kidedea baada ya kuichakaza Korea Kusini seti 3-0 za (25-12, 25-18, 25-22) katika mchezo wa fainali ya mashindano hayo ya kieneo yaliyofanyika huko Surabaya, Indonesia kuanzia Julai 23 hadi 30.
Simba na Yanga Day; Watani wang'ara
Klabu ya Simba ya Tanzania wikendi ilichuana na wageni wao APR FC ya Rwanda katika mchezo wa kirafiki ambao ulikuwa sehemu ya sherehe ya Simba Day ndani ya Dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam. Debora Fernandes na Edwin Balua ndiyo waliotikisa nyavu, Simba ikiwatandika Wanyarwanda magoli 2-0 katika mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki kuhitimisha sherehe za kilele cha maadhimisho ya miaka 88 tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo yenye makazi yake Kariakoo, Ilala.
Wakati huo huo, watani wa Simba, klabu ya Yanga siku ya Jumapili iliadhimisha Yanga Day kwa kuvaana na Red Arrows ya Zambia mbele ya mashabiki wake. Timu hizo zilikutana katika mchezo wa kirafiki wa kuhitimisha kilele cha 'Wiki ya Mwananchi', ambapo Red Arrows ilitangulia kupata bao kupitia kwa, Ricky Banda dakika ya sita kisha Mudathir Yahya kuisawazishia Yanga dakika ya 64. Bao la ushindi wa Yanga lilowanyanyua kwenye viti maelfu ya mashabiki waliokuwa wamefurika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa lilitiwa kimyani na Stephane Aziz Ki kupitia upigaji matuta katika dakika za lala salama, baada ya beki wa wageni kucheza ndivyo sivyo kwenye sanduku la hatari. Msimu mpya wa ligi unatazamiwa kuanza rasmi Agosti 8 kwa mechi itakayowakutanisha mahasimu hao wa kandanda Tanzania.
Dondoo za Olimpiki
Judoka wa Algeria amekataa kushindana na mwakilishi wa utawala haramu wa Israel katika Michezo ya Olimpiki ya Paris 2024. Messaoud Redouane Dris alichukua hatua hiyo kuwauunga mkono watu wa Palestina na kuonyesha upinzani wake dhidi ya mauaji ya kimbari yanayofanywa na Israel huko katika Ukanda wa Gaza. Idris alitakiwa kukabiliana na mwanajudo wa Kizayuni, Tohar Butbul, katika raundi ya kumi na sita, katika uzani wa kilo 73, lakini hakupunguza uzani wake ili asichuane na raia huyo wa utawala wa Kizayuni wa Israel unaoendelea kuua watoto wa Gaza. Dris anakuwa mwanajudo wa pili kutoka Algeria ambaye amejiondoa katika michuano ya Olimpiki kwa kukataa kucheza na mshindani wa Israel.
Katika hatua nyingine, mwanamasumbwi nyota mwanamke wa Kiislamu wa Australia ameijia juu Paris kwa uamuzi wake wa kuwazuia wanariadha wa Ufaransa wanaovaa vazi la staha la hijabu kushiriki katika ufunguzi na Michezo ya Olimpiki inayoendelea nchini humo.
Tina Rahimi, mwanamke wa kwanza Muislamu kuiwakilisha Australia kwenye Michezo ya Olimpiki akiwa na vazi la staha ameikosoa vikali Ufaransa kwa hatua yake hiyo aliyoitaja kuwa ya kindumakuwili na kiunfaiki. Ameandika kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii kuwa: Hupaswi kulazimika kuchagua ama imani/dini kwa upande mmoja na michezo kwa upande wa pili. Hiki ndicho wanariadha wa Ufaransa wamelazimishwa kufanya.
Mbali na hayo, timu ya soka ya wanawake ya Zambia imepigwa marufuku kushiriki Michezo ya Olimpiki kwa muda usiojulikana baada ya kumchezesha mwanamume. Timu hiyo hata hivyo ilikuwa imeshindwa vibaya katika mechi za Kundi B ambalo pia lilijumuisha Australia, Ujerumani na Marekani.
Na katika uvunaji wa medali kwenye Michezo ya Olimpiki, Marekani na China zinaongoza na kupelekana unyo kwa unyo kwenye medali za dhababu, huku Afrika Kusini ambayo kwa sasa ipo katika nafasi ya 29 ikiwa nchi ambayo kidogo imelitoa kimasomaso bara Afrika.