Sep 10, 2023 04:35 UTC
  • Rais Raisi: Iran inapinga mabadiliko yoyote katika mipaka ya eneo

Rais Ebrahim Raisi amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inapinga vikali aina yoyote ya uzushaji mivutano na kubadilishwa mipaka ya kihistoria ya eneo hili na akabainisha kwamba Tehran iko tayari kutoa mchango wa kuzuia kufanywa mabadiliko yoyote katika hali ya jiopolitiki ya eneo.

Baada ya vita vya siku 44 vilivyozuka mwaka 2020 kati ya Armenia na Jamhuri ya Azerbaijan katika eneo la Nagorno-Karabakh, nchi hizo mbili zilitia saini makubaliano ya kusitisha mapigano kwa upatanishi wa Russia; na baada ya hapo sehemu kadhaa za eneo hilo zilikabidhiwa kwa Jamhuri ya Azerbaijan; lakini licha ya kusainiwa makubaliano ya kusitisha mapigano, uhusiano kati ya nchi hizo mbili unaendelea kutawaliwa na mivutano huku kila upande ukimtuhumu mwenzake kuwa anakiuka makubaliano ya usitishaji vita.

Katika muktadha huo, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran Seyed Ebrahim Raisi jana Jumamosi alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Waziri Mkuu wa Armenia, Nikol Pashinyan, ambaye alimtaarifu kuhusu matukio ya hivi karibuni yaliyozuka katika eneo la Caucasus.

Sambamba na kusisitiza tena upinzani mkali wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa aina yoyote ya uzushaji mivutano na kubadilishwa mipaka ya kihistoria ya eneo hili, Rais Raisi alieleza utayarifu wa Iran kama jirani madhubuti wa kutoa mchango athirifu wa kuzuia kuibuka mapigano mapya na mabadiliko yoyote katika hali ya jiopolitiki ya eneo.

Seyyid Ebrahim Raisi ametangaza uungaji mkono wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa umoja wa ardhi za nchi zote za eneo na kupinga uwepo wa madola ya kigeni na akaongezea kwa kusema, masuala ya eneo inapasa yatatuliwe kwa njia ya mazungumzo na nchi zenyewe za eneo, na Tehran iko tayari kutoa mchango katika kusaidia kutatua masuala kwa njia ya mazungumzo ya kidiplomasia.

Katika mazungumzo hayo, Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan mbali na kuwasilisha ripoti ya kina kuhusu matukio ya hivi karibuni katika eneo la Caucasus Kusini na vilevile matukio yanayojiri kwenye medani ya mivutano katika eneo la Caucasus amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikitoa mchango chanya na athirifu katika kujenga, kudumisha na kuimarisha amani, utulivu na usalama katika eneo.../

 

Tags