Uchunguzi kuhusu Marekani kuitungua ndege ya abiria ya Iran
Kwa munasaba wa kukumbuka jinai ya kivita ya Marekani kuitungua ndege ya abiria ya Iran mnamo Julai 3 mwaka 1988, kumeitishwa kikao cha kujadili mitazamo ya kisheria kuhusu tukio hilo.
Kikao hicho kimefanyika leo hapa Tehran katika Jumuiya ya Kimataifa ya Amani ya Kiislamu. Dawoud Ameri, Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kimataifa ya Amani ya Kiislamu, Ali Asghar Sultaniyeh Balozi wa Zamani wa Iran katika Wakala wa Kimataifa wa Nishati ya Atomiki na Ali Ridha Sheikh Attar, Balozi wa Zamani wa Iran nchini Ujerumani ni kati ya wataalamu wa kimataifa waliozungumza katika kikao hicho.
Sultaniyeh amesema amemuandikia barua mkuu wa Shirika la Kimatiafa la Usafiri wa Angani ICAO akimtaka kuchunguza kisheria jinai hiyo ya Marekani.
Itakumbukwa kuwa miaka 28 iliyopita, ndege moja ya abiria aina ya Airbus ya Iran ilitunguliwa kwa makombora mawili ikiwa juu ya anga ya maji ya Ghuba ya Uajemi ikitokea Bandar Abbas kusini mwa Iran kuelekea Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu.
Makombora hayo yalirushwa kutoka kwenye meli za kivita za Marekani katika maji ya Ghuba ya Uajemi. Abiria wote 298 waliokuwemo ndani ya ndege hiyo wakiwemo watoto 66 waliuawa kinyama katika shambulizi hilo la kichokozi na kigaidi. Jinai hiyo ilionesha kiburi na dharau ya Marekani na jinsi nchi hiyo inavyopuuza sheria zote za kimataifa na maazimio ya kutetea haki za binadamu na kuamua kutungua hata ndege ya abiria.