Brigedia Jenerali Qaani: Israel ni dhaifu kuliko utando wa buibui
(last modified Sat, 18 Nov 2023 03:50:05 GMT )
Nov 18, 2023 03:50 UTC
  • Brigedia Jenerali Qaani: Israel ni dhaifu kuliko utando wa buibui

Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) amesema Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa imefichua kuwa utawala haramu wa Israel ni dhaifu kuliko hata nyumba ya buibui.

Brigedia Jenerali Ismail Qaani amesema hayo katika waraka aliomuandikia Kamanda wa Brigedi za Izzuddin Qassam, Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS na kuongeza kuwa: Ubunifu wenu wa Kimbunga cha al-Aqsa umeonyesha wazi udhaifu wa utawala wa Kizayuni. Utawala huu ni dhaifu hata kuliko utando wa buibui.

Brigedia Jenerali Ismail Qaani ameeleza bayana kuwa, Palestina na eneo zima la Asia Magharibi halitabaki kama lilivyokuwa baada ya Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa.

Kamanda huyo mwandamizi wa jeshi la SEPAH la Iran amemhakikishia Kamanda wa Brigedi za Izzuddin Qassam kuwa, Jamhuri ya Kiislamu itafanya kila iwezalo kuiunga mkono HAMAS katika mapambano haya ya kihistoria dhidi ya adui Mzayuni.

Amesema: Katu hatumruhusu adui katili na waungaji mkono wake kuidhibiti Gaza na wakazi azizi wa eneo hilo. HAMAS imewathibitshia watu wote kwamba, muqawama katika eneo la Gaza una uwezo mkubwa wa kimkakati na ubunifu, sambamba na kusimamia masuala ya kiuongozi na kupata ufanisi katika medani za vita.

Brigedi za Izzuddin Qassam

Kadhalika Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu amewapongeza vijana wa Palestina kwa kuendelea kupambana kishujaa na kupata ushindi mkabala wa Wazayuni.

Brigedia Jenerali Qaani amebainisha kuwa, utawala haramu wa Israel hauwezi tena kulemaza mapambano ya Wapalestina kwa risasi na silaha, na kwamba kambi ya muqawama inazalisha silaha zote inazohitaji ndani ya maeneo yake ya kijiografia.

Tags