Baqeri: Manowari ya Deylaman kudhamini usalama kaskazini mwa Iran
(last modified Mon, 27 Nov 2023 12:27:06 GMT )
Nov 27, 2023 12:27 UTC
  • Baqeri: Manowari ya Deylaman kudhamini usalama kaskazini mwa Iran

Mkuu wa Komandi Kuu ya Vikosi vya Ulinzi vya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kujiunga manowari mpya ya Deylaman kwenye orodha ya meli za kivita za Iran kutaimarisha usalama katika Bahari ya Caspian, kaskazini mwa nchi.

Meja Jenerali Mohammad Hossein Baqeri amesema hayo leo Jumatatu wakati wa hafla ya uzinduzi wa manowari hiyo mpya katika mji wa bandari wa Bandar Anzali, kaskazini mwa Iran.

Baqeri ameeleza kuwa, Bahari ya Caspian ni bahari ya amani na urafiki na kusisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ina uhusiano mzuri wa kijeshi na kiusalama na nchi zinazolizunguka bahari hilo.

Manowari ya Deylaman

Mkuu wa Vikosi vya Majeshi ya Iran amesema meli hiyo ya kijeshi imeundwa na wataalamu wa hapa nchini na kwa utaalamu wa hali ya juu, licha ya taifa hili kuwa chini vikwazo vikali na vya upande mmoja vya maadui. 

Manowari ya Deylaman ni ya tano katika safu ya meli za kivita za Jamaran, na ina uzito wa tani 1,500, na imeundwa kwa ustadi mkubwa ikilinganishwa na manowari zilizotangulia.

Kwa mara nyingine tena, Meja Jenerali Baqeri amekosoa uwepo wa kijeshi wa maajinabi katika eneo la Ghuba ya Uajemi na kusisitiza kuwa, nchi za eneo hili zina uwezo wa kujidhaminia usalama wao.

Meja Jenerali Baqeri

Naye Admeri Alireza Tangsiri, Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) amesisitiza kuwa, vikosi vya SEPAH vitaendelea kulinda maslahi ya taifa la Iran katika eneo la Ghuba ya Uajemi, ambalo lina umuhimu mkubwa kama mojawapo ya njia muhimu zaidi za baharini.

Amesema hayo katika ujumbe aliomtumia Admeri Shahram Irani, Kamanda wa Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Iran kwa mnasaba wa Siku ya Jeshi la Baharini iliyoadhimishwa leo hapa nchini.

Sehemu ya ujumbe huo inasema: "Hii leo, Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Iran na Kikosi cha Wanamaji cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) vimegeuka na kuwa nguvu kubwa ya kuzuia mashambulizi katika eneo."

Tags