Dec 30, 2023 12:09 UTC
  • Raisi: Wairani wapo macho na wanawafahamu wachochezi

Rais Ebarhim Raisi wa Iran amesema taifa la Iran linaufahamu vyema uchochezi na kuwatambua wachochezi, na ndio maana walionyesha namna wana muono wa mbali katika tukio la kihistoria la Dei 9.

Rais Raisi amesema hayo leo kwa mnasaba wa maadhimisho ya Dei 9 inayoadhimishwa leo kote nchini. Siku hii ya tarehe 9 Dei imepewa jina la "Siku ya Ung'amuzi na Muono wa Mbali" hapa nchini. 

Sayyid Raisi ameeleza bayana kuwa, maadhimisho ya Dei 9 yanapasa kutazamwa kama chimbuko la kuzalisha na kuchochea hamasa ya ung'amuzi na kusimama kidete wananchi wa Iran mkabala wa fitina na uchochezi unaopikwa na Wamagharibi.

Rais wa Iran amesema, Dei 9 ilifungua ukurasa mpya wa historia, kwa kuwa katika siku hii miaka 14 iliyopita, njama za maadui wa Mapinduzi wa Kiislamu kwa kututaka kumia madai ya wizi wa kura zilifelishwa. 

Ikumbukwe kuwa, tarehe 9 Dei mwaka 1388 Hijria Shamsia iliyosadifiana na tarehe 30 Disemba 2009, mamilioni ya wananchi wa Tehran na miji mingine hapa nchini walifanya maandamano kulalamikia machafuko ya barabarani na himaya ya madola ya Magharibi kwa ghasia hizo za wafanya fujo waliokuwa wakilalamikia matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Juni 30.

Rais Ebrahim Raisi wa Iran amesema, wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu walifuata miongozo ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya kuwataka wawe macho, na kwa msingi huo wakafanikiwa kuzima 'mapinduzi ya rangi' yaliyochochewa na Marekani hapa nchini mwaka 2009.

Raisi akihutubia katika kikao cha kumuezi mwanafalsafa maarufu wa Kiirani, Ayatullah Misbah

Baada ya uchaguzi wa Rais wa Juni 30 mwaka 2009, wagombea wawili walioshindwa walilalamikia matokeo ya uchaguzi, lakini hawakuwa tayari kufuatilia malalamiko yao kupitia njia za kisheria. Uungaji mkono wa madola ya Magharibi kwa wagombea hao ulipelekea kutokea machafuko mjini Tehran.

Kadhalika Sayyid Raisi ameashiria vita vya Israel dhidi ya Gaza na muqawama wa Wapalestina kwa zaidi ya siku 80 sasa na kubainisha kuwa, "Wasomi na wanasiasa kote duniani wanatambua kuwa, mshindi halisi katika medani ya vita ni Palestina, na Israel haijaambulia chochote isipokuwa kushindwa na kufedheheshwa."

Ameongeza kuwa, ni wazi sasa kwa dunia nzima, baada ya kupita miaka 43, msimamo wa Iran wa kuunga mkono kadhia ya Palestina na kutaka kukombolewa Quds Tukufu ni sahihi.

Tags