Amir Abdollahian: Wazayuni wanachukia vyombo vya habari
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran sambamba na kuwaenzi mashahidi wa vyombo vya habari waliouawa na Israel katika vita vya Gaza amesema: Wazayuni wanavichukia vyombo vya habari.
Hossein Amir Abdollahian ameandika kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X kwamba: "Waandishi wa habari na wapiga picha 111 wameuawa shahidi baada ya zaidi ya miezi mitatu ya vita vya kikatili dhidi ya watu wa Gaza wanaoendelewa kusimama kidete, na idadi hii ya mauaji ya waandishi habari haina kifani katika historia."
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Iran ameongeza kuwa: Wazayuni wanaogopa mno utambuzi na hukumu za walimwengu, na hii ndiyo sababu kuu ya chuki na kinyongo cha utawala huo wa kihalifu dhidi ya vyombo vya habari.
Amir Abdollahian amewaenzi waandishi habari mashahidi waliouawa na Israel na kutuma rambirambi zake kwa Bw. Wael Al-Dahdouh, mwandishi wa habari shujaa wa Palestina.
Katika jinai ya karibuni zaidi, jeshi la Israel mapema Jumapili iliyopita lilifanya mashambulizi ya anga huko Rafah na kuishambulia gari iliyokuwa imewabeba maripota wawili wa Palestina huko kusini mwa Gaza na kuwauwa shahidi.
Hamza Wael al Dahdouh ripota wa televisheni ya al Jazeera na Mustafa Thuraya mwandishi habari wa kujitegemea waliuliwa shahidi katika hujuma hiyo. Hamza ni mtoto wa ripota mkuu wa televisheni ya al Jazeera ya Qatar huko Gaza, Wael Al-Dahdouh.
Itakumbukwa kuwa baba yake Shahidi Hamza yaani Wael al Dahdouh siku kadhaa zilizopita alipoteza mke, wanawe wawili na mjukuu wake katika mashambulizi ya anga ya utawala wa Kizayuni wa Israel huko Ukanda wa Gaza.