Damu safi ya watu wa Gaza itaharakisha mkondo wa kuangamia Israel
Kamanda mkuu wa Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu Iran anasema utawala haramu wa Israel unamwaga damu ya Wapalestina wasio na hatia ili kufidia "kushindwa kwake kwa fedheha" katika vita vya Gaza, akionya kwamba ukatili huo utaharakisha mkondo wa kuangamia utawala huo.
Meja Jenerali Abdolrahim Mousavi aliyasema hayo siku ya Jumanne, baada ya kupita siku 95 za vita vya mauaji ya kimbari vya Israel dhidi ya Wapalestina katika Ukanda wa Gaza, vita ambavyo vimechafua kabisa sura ya Israel duniani.
Kamanda wa Jeshi la Iran amesema: "Chini ya uungwaji mkono wa Marekani na nchi nyingine za Magharibi, utawala haramu wa Kizayuni unalipiza kisasi kwa kuua watoto, wanawake na raia wasio na silaha wala ulinzi baada ya kupata kipigo cha kihistoria mikononi mwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas."
Aidha amesema hakuna kitakachofidia kushindwa Israel kwa fedheha na bila shaka damu iliyotakasika ya watu wa Palestina itaharakisha kuanguka kwa utawala wa Kizayuni wa Israel ambao pia ni utawala wa kibaguzi.
Israel ilianzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina kwenye Ukanda wa Gaza tarehe 7 Oktoba baada ya Hamas kutekeleza operesheni ambayo haijawahi kushuhudiwa dhidi ya utawala huo wa Kizayuni ikiwa ni katika kulipiza kisasi kwa ukatili wa utawala huo dhidi ya watu wa Palestina.
Hadi sasa utawala wa Israel imewaua Wapalestina wasiopungua 23,084 wengi wao wakiwa wanawake na watoto na kuwajeruhi wengine 58,926.
Maelfu ya wengine wametoweka na wanadhaniwa wamekufa chini ya vifusi katika Ukanda wa Gaza, ambao umezingirwa kikamilifu na Israel.