Satalaiti mpya ya Iran yatuma taarifa za kwanza kabisa ardhini
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa, satalaiti mpya zaidi ya Iran iitwayo Thuraya imefanikiwa kuunganisha mawasiliano ardhini na kutuma taarifa za awali kabisa.
Satalaiti ya Thuraya ni moja ya satalaiti mpya zaidi za Iran katika kizazi cha satalaiti za kufaniyia utafiti na ilirushwa anga za mbali Jumamosi tarehe 20 Januari 2024 kwa kutumia kombora la Qaim 100 la Iran pia. Hayo ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya wasomi na wataalamu wenye vipaji wa Iran katika Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH.
Satalaiti ya Kiirani ya Thuraya imefanikiwa kusafiri kwa mafanikio katika umbali wa kilomia 750 kutoka usawa wa bahari na hivyo kuifanya Iran iweke rekodi mpya ya kutuma satalaiti katika umbali mkubwa zaidi.
Shirika la habari la IRNA limemnukuu Isa Zarepour, Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari wa Iran akisema kuwa, mafanikio ya satalaiti ya Thuraya ya Iran, yamekamilika.
Ameongeza kuwa, mara baada ya satalaiti hiyo kufika kwenye umbali uliokusudiwa, imeanza kutuma taarifa ardhini, imeonesha eneo ilipotua na kuwezesha pia kudhibitiwa na kuendeshwa na kituo cha ardhini kilichoainishwa maalumu kwa kazi hiyo.
Huko nyuma pia wataalamu wa Iran walikuwa wamefanikiwa kubuni na kutengenezwa satalaiti nyingine kama ile ya Noor 2 na Noor 3 na kuzituma kwenye umbali wa kilomita 500 angani kutoka kwenye usawa wa bahari.
Kama tulivyosema, satalaini hii mpya ya Iran iitwayo Thuraya, imetumwa anga za mbali kwa kutumia kombora la "Qaim 100" na hiyo ni rekodi mpya ya kurushwa satalaiti na kombora hilo kwenye umbali mkubwa zaidi.