Abdollahian: Uhusiano wa Iran na Algeria upo katika mazingira bora kabisa
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, uhusiano wa taifa hili na Algeria upo katika kiwango bora kabisa.
Hussein Amir-Abdollahian amesema hayo hapa mjini Tehran kkatika mazungumzo yake na Naibu Spika wa Bunge la Algeria ambapo sambamba na kueleza kufurahishwa kwake na kuwepo ujumbe wa ngazi za juu wa Bunge la Algeria mjini Tehran amebainisha kwamba, uhusiano wa nchi hizo mbili uko katika hali bora zaidi.
Katika kikao hicho, Amir Abdollahian ameutaja mchakato wa uhusiano kati ya Iran na Algeria kuwa wenye nishati na unaoendelea kukua na kusema: Iran inatilia maanani sana upanuzi wa uhusiano na nchi za Kiafrika hususan Algeria katika siasa zake za nje na kufanyika nchini Algeria mkutano wa kilele nchi zinazouza gesi ni tukio muhimu.
Amir Abdollahian pia ameashiria utendaji mzuri na wa fakhari wa taifa la Algeria katika mapambano dhidi ya ukoloni wa Ufaransa na kupata uhuru wake, na kupongeza misimamo ya kimapinduzi na yenye misingi ya Bunge na serikali ya Algeria katika kuwaunga mkono kwa uaminifu wananchi wa Palestina na Gaza na kuitaja misimamo na hatua hizo za Algeria kuwa ni kiigizo chema kwa mataifa mengine ya Kiislamu.
Kwa upande wake Moussa Kharfi, Naibu Spika wa Bunge la Algeria sambamba na kueleza kuwa, bila shaka suala la Palestina lina umuhimu wa kistratijia kwa Algeria, na taifa la Algeria likiwa taifa la kimapinduzi lilitoa muhanga wa maisha ya zaidi ya milioni moja na nusu ili kupata uhuru kutoka kwa ukoloni wa Ufaransa, amebainisha kwamba, tuna imani kwamba Palestina itaibuka na ushindi na damu ya mashahidi haitapotea hivi hivi.