Iran yailaani Marekani kwa kuizuia UN kukomesha mauaji ya kimbari ya Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i107574-iran_yailaani_marekani_kwa_kuizuia_un_kukomesha_mauaji_ya_kimbari_ya_israel
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian ameilaani Marekani kwa kuuzuia Umoja wa Mataifa kutekeleza wajibu wake wa kushinikiza kusitishwa vita vya mauaji ya halaiki yanayoendelea kufanywa na utawala wa Israel dhidi ya wananchi wa Ghaza.
(last modified 2026-05-13T18:57:29+00:00 )
Jan 24, 2024 03:27 UTC
  • Iran yailaani Marekani kwa kuizuia UN kukomesha mauaji ya kimbari ya Israel

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian ameilaani Marekani kwa kuuzuia Umoja wa Mataifa kutekeleza wajibu wake wa kushinikiza kusitishwa vita vya mauaji ya halaiki yanayoendelea kufanywa na utawala wa Israel dhidi ya wananchi wa Ghaza.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iran amesema hayo leo Jumatano wakati akihutubia kikao cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Asia Magharibi hususan Ghaza.

Utawala wa Kizayuni wa Israel ulianzisha vita vya kikatili tarehe 7 Oktoba 2023 dhidi ya wanawake, watoto wadogo na raia wa kawaida wa Ghaza huko Palestina kufuatia operesheni ya kimbunga ya al-Aqsa ya harakati za muqawama za Ghaza. Takriban Wapalestina 25,500, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wameshauawa shahidi hadi hivi sasa kutokana na mashambulizi hayo ya kikatili ya Israel.

Wahanga wakuu wa jinai za Israel huko Ghaza ni wanawake na watoto wadogo

 

Marekani ndiye mdhamini mkuu wa silaha kwa Israel na mbali na uungwaji mkono wa kijeshi na kisiasa usio na masharti katika mashambulizi yake dhidi ya Ghaza, Washington imeisheheneza Tel Aviv zaidi ya tani 10,000 za zana za kijeshi ili izidi kuua kikatili wananchi wa Palestina. Marekani pia imekuwa ikipigia kura za veto na kuzuia maazimio yote yaliyo dhidi ya Israel kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na ndiyo inayochochea kuendelea jinai za utawala wa Kizayuni huko Palestina. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameilaani Marekani kwa kuitumikia Israel kibubusa na kushiriki kikamilifu katika mauaji ya umati wanayofanyiwa Wapalestina.

Katika hotuba yake ya leo Jumatano mbele ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, Amir-Abdollahian amesema, Washington inauzuia Umoja wa Mataifa kutekeleza majukumu yake ya asili katika kukomesha mauaji ya halaiki yanayofanywa na Israel ina inakwamisha juhudi zote za kukomeshwa vita kwenye Ukanda wa Ghaza."

Amesema: "...Marekani lazima iulazimishe utawala wa Kizayuni ukomeshe vita ili kwa njia hiyo iweze kujiondoa kwenye mtego ambao utawala wa Israel umeuweka ili kuiingiza Marekani kwenye migogoro ya moja kwa moja."