Mabalozi wa Iran na Pakistan warejea katika vituo vyao vya kazi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i107670-mabalozi_wa_iran_na_pakistan_warejea_katika_vituo_vyao_vya_kazi
Mabalozi wa Iran na Pakistan ambao walikuwa wamerejea makwao baada ya mzozo ulioibuka hivi karibuni baina ya mataifa haya mawili, hatimaye jana walirejea katika vituo vyao vya kazi.
(last modified 2024-01-26T23:05:56+00:00 )
Jan 26, 2024 23:05 UTC
  • Mabalozi wa Iran na Pakistan warejea katika vituo vyao vya kazi

Mabalozi wa Iran na Pakistan ambao walikuwa wamerejea makwao baada ya mzozo ulioibuka hivi karibuni baina ya mataifa haya mawili, hatimaye jana walirejea katika vituo vyao vya kazi.

Baada ya shambulio la Iran kwenye makao makuu ya magaidi nchini Pakistan na shambulio kama hilo la Pakistan katika maeneo kadhaa ya mpaka wa Iran, ambayo kwa mujibu wa serikali ya nchi hii yalikuwa makazi ya magaidi wa Pakistan, kivuli cha suutahafahamu kilitanda kwa muda mfupi katika uhusiano mkongwe wa nchi hizi mbili muhimu za Kiislamu, lakini mamlaka nchi hizo mbili zilisisitiza haja ya kuzuia kuongezeka kwa mvutano, na kisha Islamabad ikatangaza kufikiwa makubaliano na Tehran ili kupunguza mvutano katika uhusiano wa pande mbili.

Jumatatu ya wiki hii, Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran na Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Pakistan zilitoa taarifa ya pamoja inayosema kuwa, kufuatia mazungumzo ya simu kati ya Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Iran na Pakistan, pande hizo mbili zimekubaliana kuwa mabalozi wa nchi hizo mbili watarejea katika vituo vyao vya kazi ifikapo Januari 26.

Bendera za Iran na Pakistan

 

Hatimaye jana Ijumaa mabalozi hao walirejea katika vituo vyao vya kazi na hivyo kuufanya uhusiano wa kidiplomasia kati ya Pakistan na Iran ambao ulikaribia kuharibika kurejea katika hali yake ya kawaida.

Kurejeshwa kwa uhusiano wa Iran na Pakistan katika hali ya kawaida kunatimia katika hali ambayo, baadhi ya pande zinazonufaika na mvutano na kufifia uhusiano kati ya Tehran na Islamabad zilikuwa zikijaribu kuzidisha hali ya wasiwasi kwa kulikuza na kuangazia suala la hatua ya kijeshi ya Iran dhidi ya magaidi nchini Pakistan na hivyo kuchochea moto wa fitina katika uhusiano kati ya nchi hizo mbili na kuichukulia hatua hiyo ya Iran kama utanuaji misuli dhidi ya majirani zake.