22 Bahman mahudhurio ya hamasa ya Wairan na sisitizo la kusimama kidete
Jumapili ya jana, tarehe 22 Bahman (Februari 11) ilisadifiana na maadhimisho ya mwaka wa 45 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Mwaka huu, kama ilivyokuwa miaka iliyopita, wananchi wa Iran walikuwa na mahudhurio makubwa na ya hamasa katika maandamano ya Yaumullah 22 Bahman katika mikoa tofauti ya Iran.
Mahudhurio makubwa na mshikamano wa wananchi wa Iran katika maandamano ya 22 ya Bahman katika kipindi cha miaka 45 iliyopita yamegeuka na kuwa nembo ya kusimama kidete, umoja na sherehe za ushindi wa taifa la Iran dhidi ya mfumo wa kibeberu.
Siku hii ya kitaifa ni ukumbusho wa moja ya matukio makubwa ya kihistoria ya taifa la Iran; taifa ambalo limeingia mitaani katika kipindi cha miaka 45 katika hali yoyote ile na kuonyesha umoja na mshikamano wake kwa ulimwengu katika kulinda thamani za mapinduzi.
Katika miaka hii, mashambulizi ya mabomu ya adui wa Kibaath katika miaka minane ya vita vya kulazimishwa vya Iraq dhidi ya Iran, mashinikizo ya kisiasa navikwazo vya kiuchumi ya Marekani na waitifaki wake ni mambo ambayo hayakuweza katu kutia dosari azma na irada ya taifa la Iran la kuendeleza njia ya mapinduzi.
Ushiriki wa wananchi katika matembezi ya maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni uwanja wa mwamko na umakini wao, umoja wao na uelewa wao, na kutilia maanani hatima ya nchi na kutangaza kuchukizwa kwao na maadui wa nchi. Mfumo wa Kiislamu ambao umekuwa chimbuko la faraja kwa marafiki wa mfumo wa Kiislamu na kusambaratisha njama za maadui wa ndani na wa nje wa mapinduzi hayo.
Washiriki wa matembezi ya mwaka huu ya Yaumullah 22 Bahman, wakizingatia hali nyeti za nchi na eneo kutokana na duru mpya ya hujuma ya kijeshi ya utawala wa Kizayuni katika ardhi ya Palestina na waungaji mkono wake katika eneo hili, katika azimio lao mwishoni mwa maandamano hayo sambamba na kujadidisha tena utiifu wao kwa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Imam Ruhullah Khomeini (RA) na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu wamesema: Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yameweka roho mpya katika mwili wa Umma wa Kiislamu, na sambamba na kupanua mapambano ya kupinga dhulma na nyanja za makabiliano ya kimkakati na mfumo wa kibeberu nje ya ya jiografia ya Iran ya Kiislamu, yamefungua ukurasa mpya kwa jamii ya wanadamu na kutoa bishara njema ya kujitokeza mfumo mpya wa kimataifa".
Katika azimio hilo, washiriki wameutaja umoja, mshikamano na maelewano ya kitaifa katika mhimili wa utawala wa faqihi na Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi kuwa ni wadhamini wakuu na vichochezi vya ushindi wa Iran ya Kiislamu kwa ajili ya kuvuka migogoro, fitna na changamoto zinazosababishwa na njama za maadui wa kigeni na watu wasiolitakia mema taifa, ndani ya nchi.
Rais Sayyid Ebrahim Raisi aliashiria katika hotuba yake mbele ya umati mkubwa wa waandamanaji waliokusanyika mjini Tehran kuadhimisha mwaka wa 45 wa ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza na misaada na himaya ya Marekani kwa utawala huo na kutilia mkazo udharura wa kusitishwa haraka mashambulizi ya utawala wa Kizayuni dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza huko Palestina.
Amesema: Licha ya njama zisizosita za Wamagharibi, Iran inaendelea kuiunga mkono Palestina na fikra za Mapinduzi ya Kiislamu, na baada ya miaka 45 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu imethibitika kuwa, haki iko upande wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Imam Ruhullah Khomeini ambaye alisema Palestina ndiyo kadhia nambari moja ya Umma wa Kiislamu na kwamba Quds lazima ikombolewe.
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, njia ya kuuangamiza utawala wa Kizayuni na kukomesha jinai zake ni kukata uhusiano na milingano yote ya kiuchumi na utawala huo ghasibu.
Rais Ebrahim Raisi sambamba kuashiria kwamba, maendeleo ya Iran ya Kiislamu yamepatikana katika kivuli cha kumwamini na kumtegemea Mwenyezi Mungu na kujiamini, na katika muktadha huu Iran imeshika nafasi ya 15 ya maendeleo ya kisayansi duniani ameeleza kwamba, kwa baraka za Mapinduzi ya Kiislamu na juhudi za vijana, Iran sasa ni miongoni mwa vinara wa dunia katika nyuga za tiba, bioteknolojia na nanoteknolojia.
Ni dhahiri kwamba Mapinduzi ya Kiislamu yamekuwa na nafasi si tu kwa wananchi wa Iran na Waislamu wa nchi nyingine, bali pia kuwa kigezo cha wapenda uhuru duniani. Kwa muktadha huo, maandamano ya hamasa ya 22 Bahman yanakumbusha thamani, malengo aali na uundaji wa ustaarabu wa kisasa wa Kiislamu kwa ajili ya Waislamu wote na watu wanaopigania uhuru wa ulimwengu.
Mahudhurio yenye welewa na ya daima ya wananchi wa Iran katika medani mbalimbali za Mapinduzi ya Kiislamu yakiwemo matembezi ya mwaka huu ya tarehe 22 Bahman ni kutuma ujumbe huu kwa walimwengu hususan Marekani kwamba Mapinduzi ya Kiislamu yana rasilimali ya kijamii na ya uhakika ambayo chini ya kivuli hicho na licha ya njama zote, Mapinduzi ya Kiislamu yanaadhimisha mwaka wa 45 wa ushindi wake tangu yalipotokea mwaka 1979 kwa uuongozi wa Imamu Khomeini (MA).