Feb 17, 2024 11:34 UTC
  • Iran yazindua mifumo mipya ya ulinzi ya kukabili makombora

Jeshi la Iran limezindua mifumo mipya ya kistratijia katika sekta za makombora na ulinzi wa anga.

Shirika la habari la IRNA limeripoti habari hiyo na kuongeza kuwa, Iran leo Jumamosi imezindua mfumo mpya wa kukabiliana na makombora ya balestiki wa 'Arman' na mfumo wa ulinzi wa anga wa “Azarakhsh”.

Kwa mujibu wa IRNA, mifumo hiyo mpya iliyozinduliwa leo itapiga jeki mifumo ya ulinzi wa anga ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Uzinduzi huo umefanyika mbele ya Waziri wa Ulinzi wa Iran, Brigedia Jenerali Mohammad Reza Ashtiani.

Makombora yanayotumika katika mfumo wa ulinzi wa Arman ni katika familia ya mfumo wa anga wa Sayyad-3, uliotengenezwa kwa mujibu wa vigezo vya teknolojia mpya kabisa duniani na unaweza kukabiliana na kutungua ndege za kivita zisizoonekana na rada, ndege zisizo na rubani, makombora ya cruise, helikopta na kadhalika. 

Mfumo mpya wa kukabiliana na makombora ya balestiki wa 'Arman'

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesisitiza kuwa, wizara hiyo itaendelea kuimarisha uwezo wa jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa nguvu zake zote, licha ya taifa hili kuwa chini ya mashinikizo ya maadui.

Uzinduzi wa mifumo na vifaa hivyo vya ulinzi ni matokeo ya juhudi za wanasayansi na wataalamu wa viwanda vya ulinzi vya majeshi ya Iran pamoja na kampuni za sekta binafsi, na vituo maalum vya Vikosi vya Ulinzi vya Iran.

Ifahamike kuwa, doktrini ya kiulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imejengeka katika msingi  wa kutegemea uwezo mkubwa wa nguvu kazi ya ndani ya nchi.

Tags