Kuchaguliwa wagombea wanaofaa, mdhamini wa maslahi ya taifa
Sambamba na kufanyika leo tarehe Mosi Machi uchaguzi wa awamu ya kumi na mbili ya Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu na awamu ya sita ya Baraza la Wataalamu Wanaomchagua Kiongozi Muadhamu, suala la kuchagua wagombea wanaofaa ni moja ya nukta muhimu ambazo zimekuwa zikitiliwa mkazo na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika uchaguzi huu na chaguzi nyingine zote zilizopita.
Kushiriki wananchi katika uchaguzi, licha ya kuwa ni haki ya raia kwa ajili ya kujiamulia hatima yao wenyewe katika mfumo wa Kiislamu, pia ni wajibu wao wa kidini, kwa sababu katika Uislamu popote pale panapokuwa na haki ya mtu, pia pana wajibu kwake kuhusiana na haki hiyo.
Kutokana na kuwa mwanadamu analazimika kuchukua maamuzi bora zaidi katika kutekeleza majuhumu yake ya kidini, hivyo, licha ya kulazimika kushiriki katika uchaguzi, pia anapaswa kutoa umuhimu kwa suala la kuwachagua wagombea wanaofaa katika uchaguzi huo.
Katika matamshi yake mbalimbali tofauti, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu daima amekuwa akiashiria umuhimu wa wananchi kuwa makini katika kuwachagua wagombea, na kubainisha vigezo kama vile mtu kuwa na misingi ya kidini, mwamko wa kisiasa, ujasiri na ushupavu katika kukabiliana na masuala mbalimbali, kufahamu masuala ya nchi pamoja na ya kimataifa kuwa miongoni mwa mambo yanayopaswa kuzingatiwa wakati wa kuchunguza na kutathmini wagombea wanaofaa katika uchaguzi.
Jumatano pia katika kikao na maelfu ya vijana ambao itakuwa ni mara yao ya kwanza kushiriki katika uchaguzi na vilevile familia za mashahidi, Ayatollah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu pamoja na kubainisha vigezo vya wagombea waliopitishwa na Baraza la Katiba na kamati ya kusimamia uchaguzi kuwa sahihi, alisema: Mgombea aliye bora zaidi ni yule anayeshikamana na dini kivitendo na kuheshimu sheria za kidini, anayetoa kipaumbele kwa suala la uhuru wa nchi na kutofungamana na wageni, kuwa mstari wa mbele katika kupambana na ufisadi, yuko makini zaidi kuhusiana na maslahi ya taifa na kufadhilisha ustawi na maendeleo ya nchi kuliko maslahi ya mtu binafsi na ya kichama.
Bila shaka uchaguzi ni mojawapo ya mambo yanayoimarisha mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na pia ni kizuizi cha kufikiwa malengo ya maadui. Kwa hivyo kushiriki kwa wingi wananchi katika chaguzi kunadhamini usalama na maslahi ya kitaifa. Kwa maneno mengine ni kwamba, kwa kuwa uchaguzi ni moja ya vipengele vinavyodhamini utulivu wa mfumo wa kisiasa, uadilifu na maslahi ya umma kitaifa, hivyo, kufanyika uchaguzi kwa shauku, mbali na kudhamini masuala ya ndani, pia kunaimarisha uwezo na nguvu na kuboresha itibari ya nchi kimataifa.

Kwa hiyo, kushiriki kwa wingi wananchi katika uchaguzi na kuwachagua viongozi wanaofaa kunaimarisha misingi ya mfumo wa kiislamu, imani ya wananchi na kuwakatisha tamaa maadui wa taifa hili.
Katika mazungumzo yake hayo ya Jumatano, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu alikutaja kushiriki kwa hamasa na nguvu zote wananchi katika uchaguzi, kuwa ni dhihirisho la uwezo wa taifa, hakikisho la usalama wa taifa na alama ya kuwakatisha tamaa maadui ambao wanaitazama Iran kwa jicho la tamaa. Amesisitiza kuwa, kufanyika uchaguzi kwa hamasa kunaandaa uwanja wa kutatuliwa matatizo ya nchi, na kwamba ni nguzo ya maendeleo na utawala bora na kuwa yeyote anayeipenda Iran, Jamhuri ya Kiislamu, Mapinduzi, nguvu na maendeleo ya taifa hili, bila shaka ameshiriki katika uchaguzi wa leo Ijumaa.