Global Firepower: Iran ni nchi ya 14 kwa nguvu za kijeshi duniani
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetajwa kuwa nchi ya 14 duniani kwa nguvu za kijeshi.
Hayo yamo katika ripoti ya Global Firepower, ambayo ni tovuti maalumu ya kijeshi kwa kuorodhesha nguvu za kijeshi za nchi 145 kwa kuzingatia zaidi ya viashirio 60.
Ripoti ya Global Firepower imeiweka Iran nafasi ya 14 duniani miongoni mwa nchi zenye uwezo na nguvu kubwa za kijeshi.
Nafasi hii inatokana na idadi inayojulikana kama "Global Firepower Index", ambayo inakokotolewa kwa kuzingatia zaidi ya vipengele 60, ikiwa ni pamoja na idadi ya vitengo vya kijeshi, hali ya kiuchumi, uwezo wa usaidizi na vipengele vya kijiografia.
Katika nafasi orodha hiyo, nchi za Marekani, Russia, China zinashika nafasi ya kwanza hadi ya tatu. Aidha nchi za India, Korea Kusini, Uingereza, Japan, Uturuki, Pakistan na Italia zimeorodheshwa kushikilia nafasi ya nne hadi ya kumi mtawalia.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezipiku nchi nyingi katika orodha hiyo ya mataifa yenye nguvu za kijeshi duniani licha ya kuandamwa na vikwazo vya kila upande vya Marekani na washirika wake wa Magharibi.
Katika miaka ya hivi karibuni Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imepata maendeleo yanayohisika na kuonekana katika uga wa ulinzi na kijeshi, kiasi kwamba, hii leo Iran ni nchi ya tano kwa uzalishaji wa ndege zisizo na rubani (droni) zisizoonekana na rada na nchi ya kumi duniani kwa kuzalisha manowari.