Raisi: Afrika ina nafasi muhimu katika sera ya nje ya Iran
Rais Ebrahim Raisi wa Iran ameeleza kuwa Afrika ina nafasi muhimu katika sere za nje za serikali yake na akasema: "Suala la kuwa na mahusiano na Afrika kwa ujumla, hususan nchi za Kiislamu barani humo lina nafasi ya pekee sana katika sera yetu ya mambo ya nje."
Rais Sayyid Ebrahim Raisi amesema haya leo asubuhi kabla ya kuondoka hapa Tehran kuelekea Algeria na kueleza kwamba: "Awali ya yote, tunapaswa kumshukuru Mwenyezi Mungu kutokana na ushiriki mkubwa wa wananchi katika uchaguzi; sina budi kuwashukuru wananchi kwa kutambua nyakati na wajibu wao".
Kuhusu ziara yake nchini Algeria, Rais Ebrahim Raisi amesema kuwa, ziara hiyo inafanyika kufuatia mwaliko wa Rais wa Algeria kwa ajili ya kushiriki katika Mkutano wa Saba wa Wakuu wa Nchi Zinazouza Gesi Duniani (GECF). Ameongeza kuwa, masuala mawili yamezingatiwa katika ziara hiyo, la kwanza likiwa ni mazungumzo ya pande mbili katika ngazi ya marais wa nchi ambapo ni miaka 16 sasa ziara kama hii haijafanyika.
Rais wa Iran amesema kuwa Wairani wanaitazama Algeria kama nchi iliyopambana dhidi ya wakoloni na wana kumbukumbu nzuri sana kuhusu mapambano na harakati imara za wananchi wa Algeria dhidi ya wakoloni.
Rais Ebrahim Rais aliendelea kusema kuwa: Algeria ina nafasi maalumu barani Afrika na kwamba nchi hiyo ipo katika ukanda wa utamaduni wa Kiislamu. "Uhusiano wetu na Algeria unasaidia sana uhusiano wetu na Afrika; na nafasi ya nchi hizi mbili katika OPEC ya mafuta na gesi na katika Ulimwengu wa Kiislamu inazikurubisha zaidi nchi mbili, amesema Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.