Haki halali na ya kisheria ya Iran kujibu jinai za Wazayuni
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i110510-haki_halali_na_ya_kisheria_ya_iran_kujibu_jinai_za_wazayuni
Wawakilishi wa nchi 121 wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM mjini New York wametoa taarifa wakilaani hujuma ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya maeneo ya kidiplomasia na wawakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus Syria, na kutangaza mshikamano wao na wananchi, serikali ya Iran na familia za wahanga wa shambulio hilo.
(last modified 2024-04-11T04:57:20+00:00 )
Apr 11, 2024 04:57 UTC
  • Haki halali na ya kisheria ya Iran kujibu jinai za Wazayuni

Wawakilishi wa nchi 121 wanachama wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM mjini New York wametoa taarifa wakilaani hujuma ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya maeneo ya kidiplomasia na wawakilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus Syria, na kutangaza mshikamano wao na wananchi, serikali ya Iran na familia za wahanga wa shambulio hilo.

Kufuatia kushindwa mfululizo utawala wa Kizayuni katika kukabiliana na wapiganaji wa muqawama katika eneo, Jumatatu ya tarehe Mosi Aprili utawala huo ulitekeleza jinai mpya ambapo ulituma ndege zake za kivita kwenda kushambulia jengo la ubalozi mdogo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus. Kufuatia shambulio hilo la kigaidi Brigedia Jenerali Mohammad Reza Zahedi na Brigedia Jenerali Mohammad Hadi Haji Rahimi makamanda na maveterani wa vita vya kujitetea kutakatifu, washauri wa kijeshi wa Iran huko Syria, na maafisa 5 walioandamana nao waliuawa shahidi.

Mashambulizi ya utawala wa Kizayuni katika jengo la ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus yameibua wimbi la ukosoaji katika ngazi za kieneo na kimataifa, ambapo serikali nyingi zimelaani shambulio hilo la kichokozi na kigaidi linalokiuka sheria za kimataifa.

Taarifa ya wawakilishi wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote mjini New York, inaeleza kuwa mashambulizi hayo dhidi ya maeneo na wawakilishi wa kidiplomasia hayawezi kuhalalishwa kwa namna yoyote ile na ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa pamoja na Hati ya Umoja wa Mataifa. Inasisitiza kwamba uhalifu huo ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimsingi zinazolinda maeneo na wawakilishi wa kidiplomasia chini ya Mkataba wa Haki za Kidiplomasia (1961), Mkataba wa Haki za Kibalozi (1963) na Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu Dhidi ya Watu Wanaolindwa Kimataifa wakiwemo Wawakilishi wa Kidiplomasia (1973).

Shambulio la Wazayuni dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus

Ni wazi kwamba shambulio la Wazayuni dhidi ya ubalozi mdogo wa Iran mjini Damascus ni ukiukaji wa mikataba yote ya Vienna, ambayo inasisitiza kuwa hakuna mtu wala nchi yoyote iliyo na haki ya kushambulia maeneo na vituo vya kidiplomasia na kibalozi. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndipo serikali ya Marekani ikawa inajaribu kufanya kila inaloweza kijitenga na shambulio hilo ili kuepuka matokeo yake ya kisiasa, kidiplomasia na kisheria. Lakini ikumbukwe kwamba kimsingi uhai wa utawala wa Kizayuni na vitendo vyake vyote vya kigaidi vinavyochochea mvutano na ghasia katika eneo vinatokana na uungaji mkono usio na masharti wa Washington kwa utawala huo ghasibu. Upinzani wa Marekani na nchi mbili za Ulaya za Uingereza na Ufaransa dhidi ya kutolewa tamko la kulaani shambulio hilo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni ishara ya wazi kwamba Marekani inaunga mkono jinai hiyo ya utawala wa Kizayuni.

Ikumbukwe kwamba kwa mujibu wa sheria za kimataifa, nchi inaposhambuliwa, inaruhusiwa kuchukua hatua yoyote kujitetea, na kwa vile maeneo ya kidiplomasia yana kinga ya kisheria na kuchukuliwa kuwa sehemu ya ardhi ya nchi iliyolengwa, hivyo iwapo itashambuliwa kijeshi, haswa na upande wa tatu, nchi hiyo ina haki ya kisheria ya kujitetea.

Jamhuri ya Kiislamu ya Iran sambamba na kuiwajibisha Marekani kutokana na jinai iliyofanywa na Wazayuni katika kushambulia ubalozi wake mdogo huko Syria, inasisitiza juu ya kukabiliana na jinai hiyo na inaona kuwa ni haki yake ya kisheria kujilinda na wakati huo huo kuwaadhibu Wazayuni waliotenda jinai hiyo.

Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran akiwemo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wametangaza wazi udharura wa kulipiza kisasi cha shambulio hilo hatari la anga dhidi ya jengo la ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria.

Ayatullah Khamenei katika khutba aliyotoa katika Swala ya Eid al-Fitr jana Jumatano mjini Tehran akizungumzia shambulio hilo la utawala wa Kizayuni amesema: "Kwa mujibu wa sheria za kimataifa, kushambuliwa ubalozi mdogo na ubalozi wa nchi yoyote ile ni kushambuliwa ardhi ya nchi hiyo, hivyo utawala khabithi wa Kizayuni uliozama kwenye jinai lazima uadhibiwe kutokana na jinai hiyo."