Alavi: Iran imewatia nguvuni magaidi 6
Waziri wa Upelelezi wa Iran amesema kuwa vyombo vya upelelezi hapa nchini havitatoa mwanya kwa yeyote kuvuruga usalama wa Iran na wananchi wake.
Sayyid Mahmoud Alavi amewaambia wandishi habari mjini Tehran kwamba mwishoni mwa mwezi mtukufu wa Ramadhani wizara hiyo iliwatia nguvuni wanachama tano hadi sita wa makundi ya kigaidi waliokuwa na nia ya kufanya mashambulizi ya kigaidi hapa nchini. Amesema kuwa magaidi hao walipanga kufanya mashambulizi ya kigaidi katika usiku wa Lailatul Qadr na katika maandamano ya Siku ya Kimataifa ya Quds katika miji mbalimbali ya Iran.
Waziri wa Upelelezi wa Iran pia ameashiria mkutano wa kundi la kigaidi la MKO uliofanyika hivi karibuni mjini Paris, Ufaransa na kusema kundi hilo halina ubavu na kwamba mkutano huo ni kielelezo cha kukata tamaa maadui wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ikiwemo Saudi Arabia ambayo inafanya jitihada za kuidhuru Iran kwa kutumia mbinu zote lakini hadi sasa imefeli.
Mkuu wa zamani wa vyombo vya upelelezi vya Saudi Arabia, Turki al Faisal alihudhuria katika mkutano wa Paris ulioitishwa na kundi la kigaidi la MKO lililohusika na mauaji ya maelfu ya raia nchini Iran.