Apr 29, 2024 06:43 UTC
  • Kuongezeka mauzo ya nje ya bidhaa zisizokuwa za mafuta za Iran

Maonesho ya 6 ya uwezo wa kuuza nje bidhaa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran yalianza Jumamosi hapa mjini Tehran kwa hotuba ya Rais Ebrahim Raisi.

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameyataja maonesho haya kuwa dhihirisho la uwezo wa uzalishaji na uuzaji nje bidhaa za Iran na kueleza matumaini yake kuwa matokeo ya maonyesho haya yatakuwa ni kuandaliwa uwanja na mazingira ya ushindani kwa ajili ya kuboresha ushirikiano na maingiliano ya kieneo na kimataifa kupitia ustawi wa kibiashara, upanuzi wa maingiliano ya kiuchumi, ambayo yatapelekea kuimarika umoja, mfungamano  na ushiriki wa sekta zote za kiuchumi na hivyo kuboreka  uchumi wa Iran, kieneo na kimataifa.

Maonyesho ya 6 ya Uwezo wa Kuuza Nje Bidhaa za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran (Expo 2024) yameshirikisha maafisa wa kisiasa 198 na zaidi ya wafanyabiashara 2,000, wawekezaji na wafanyabiashara wa kigeni kutoka takriban nchi 100 ulimwenguni.

Maonyesho hayo muhimu na ya kimkakati, na ambayo yataendelea hadi Mei mosi yanatambulisha bidhaa na mafanikio ya Iran katika nyanja mbalimbali za viwanda na kilimo katika makundi saba ya bidhaa, ikiwa ni pamoja na sekta ya magari na utengenezaji wa vipuri, sekta ya chakula, kilimo na uvuvi, viwanda, mazulia, kazi za mikono na utalii, dawa, vifaa vya matibabu, maabara, kemikali, vipodozi na bidhaa za afya, sekta ya ujenzi na uhandisi wa kiufundi na huduma za petrokemikali.

Maonyesho haya yametoa fursa kwa wazalishaji wa ndani kuonesha bidhaa na mafanikio yao na kuzithibitishia nchi nyingine kwamba Iran imepata mafanikio makubwa licha ya kuwekewa vikwazo vya kidhalimu na kwa busara imegeuza vitisho kuwa fursa za kudumu na endelevu.

Kile ambacho maonyesho haya yanakifuatilia na kimeweza kuonekana wazi katika siku ya kwanza ya maonyesho haya, ni kuepusha uchumi wa nchi kutegemea mapato ya mafuta. Kama Alivyoashria Abbas Aliabadi, Waziri wa Viwanda, Madini na Biashara wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, katika ufunguzi wa maonesho hayo, kiwango cha biashara ya nje ya Iran, ikiwa ni pamoja na mauzo ya nje ya bidhaa zisizo za mafuta, mauzo ya mafuta na uagizaji wa bidhaa nchini, kimefikia dola bilioni 153, ambapo karibu dola bilioni 50 zinatokana na mauzo ya nje ya bidhaa zisizokuwa za mafuta. Jambo hili linaonyesha kwamba angalau thuluthi moja ya biashara ya nje ya Iran inahusiana na mauzo ya nje yasiyo ya bidhaa za mafuta, suala linaloonyesha wazi kushindwa mradi wa maadui wa kuiwekea Iran vikwazo vya kulemaza. Katika uchumi wa kisasa, kiwango cha maendeleo ya nchi hutegemea moja kwa moja kiasi cha mahusiano ya biashara ya kimataifa ya nchi hiyo.

Rais Ebrajim Rais akizungumza katika ufunguzi wa maonyesho hayo ya Iran Expo

Kwa hiyo, ustawi wa mauzo ya nje na upatikanaji wa rasilimali za fedha za kigeni ni miongoni mwa malengo muhimu ya watunga sheria. Kwa kuingia madarakani serikali ya 13, mahusiano ya kiuchumi na kibiashara ya Iran na nchi za Afrika, China, Russia n.k yameimarika sana na hivyo kuongeza pakubwa mauzo yake ya nje ya bidhaa zisizokuwa za mafuta.

Miongoni mwa mambo yenye ufanisi mkubwa katika uwanja huu ni kutekelezwa hati ya ushirikiano wa kistratijia wa miaka 25 kati ya Iran na China, ongezeko la asilimia 200 la mabadilishano ya kibiashara na Venezuela na kuongezeka maradufu kiwango cha biashara kati ya Iran na bara la Afrika.

Kutoa kipaumbele kwa diplomasia ya uchumi kwa lengo la kuendeleza uwekezaji wa kigeni, kuingia katika masoko ya nje kwa ajili ya kupata teknolojia mpya, maingiliano chanya na nchi za kikanda kwa ajili ya kunufaika na teknolojia na ushirikiano wa viwanda, kunufaika zaidi na mahusiano ya kisiasa katika kubuni masoko mapya na maendeleo ya mitandao ya usambazaji bidhaa, kuongeza washauri wa kibiashara kwa ajili ya kufuatilia washindani wa Iran katika masoko ya dunia na kutoa taarifa muhimu kwa wafanyabiashara kwa ushirikiano wa Wizara ya Mambo ya Nje, kubadilishana mbinu za biashara kama vile matumizi ya fedha za ndani na maendeleo ya masoko ya mipakani ili kuongeza mauzo ya nje na kuboresha upatikanaji wa rasilimali nje ya nchi, kutumia uwezo wa vyumba vya pamoja vya biashara na vyama vya sekta binafsi katika maendeleo ya mahusiano na upanuzi wa masoko ya nje ni njia nyingine za kufanikisha ustawi wa mauzo ya nje ya bidhaa zisizotokana na mafuta.

Hata hivyo, mambo muhimu zaidi yanayoathiri mauzo ya nje ya bidhaa zisizo za mafuta kwa muda mrefu ni uzalishaji ghafi wa ndani na bei nafuu ya bidhaa zinazouzwa katika masoko ya dunia, na kwa kuzingatia kuwa mwaka huu umepewa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu jina la mwaka wa "Kuimarishwa Uzalishaji kwa Kushirikishwa Wananchi,"  kuna matumaini kwamba mauzo ya nje ya Iran ya bidhaa zisizo za mafuta yataongezeka zaidi mwaka huu kuliko miaka iliyopita.