Azma ya Iran ya kuimarisha ushirikiano na nchi za eneo
Hossein Amirabdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza katika kikao cha tatu cha mazungumzo ya Iran na nchi za Kiarabu kwa ajili ya maingiliano na ushirikiano kwamba Iran imeazimia kuboresha na kuimarisha maelewano na ushirikiano kati yake na nchi za eneo.
Kikao cha tatu cha mazungumzo ya Iran na nchi za Kiarabu kwa ajili ya kuimarisha maelewano na ushirikiano kilifanyika Jumapili, Mei 12, kwa hotuba ya Hossein Amirabdollahian, Waziri wa Mashauri ya Kigeni na kuhudhuriwa na wanafikra na shakhsia wa kisiasa, kwa usimamizi wa Baraza la Kistratejia la Mahusiano ya Kigeni hapa mjini Tehran.
Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran alisema katika kikao hicho: 'Kwa kuzingatia sera zake za ujirani mwema, Iran imefanya juhudi kubwa za kujistawisha pamoja na majirani zake wote na ulimwengu wa Kiislamu na Kiarabu, na mfano wa hilo ni hatua za kurejeshwa uhusiano wa kawaida kati ya Riyadh na Tehran.
Kuhusu mpango wa Iran kuhusiana na kadhia ya Palestina, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa: 'Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwasilisha mpango wa kidemokrasia wa kufanyika kura ya maoni miaka kadhaa iliyopita na kusajiliwa katika Umoja wa Mataifa kama suluhisho la kisiasa la mgogoro huo, ambapo mgogoro wa Palestina unapaswa kuwa kitovu cha mazingatio ya ulimwengu wa Kiislamu.'
Katika miaka ya hivi karibuni, Viongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima wamekuwa wakitoa kipaumbele muhimu katika siasa zao za kigeni kwa suala la kuimarishwa uhusiano na majirani zake. Iran imekuwa na nafasi muhimu na madhubuti katika kuimarisha amani, uthabiti na usalama wa eneo, ambapo uwepo wa jeshi lake lenye nguvu kwa namna fulani umeleta utulivu na kupunguza mivutano katrika eneo.
Nafasi ya vyombo vya usalama na jeshi la Iran imetoa mchango mkubwa katika kukabiliana na harakati za makundi ya kigaidi, ambapo operesheni za jeshi lake zimepelekea kufeli njama za makundi hayo na ya waungaji mkono wao wa nchi za Magharibi katika kuibua mivutano na ukosefu wa usalama katika eneo.
Katika miaka ya hivi karibuni Marekani na serikali za Ulaya zimechangia pakubwa katika kuvuruga amani na uthabiti wa eneo kwa kuyaunga mkono makundi ya kigaidi, ambapo uingiliaji wa jeshi la Marekani nchini Iraq, Afghanistan na Syria ulivuruga pakubwa usalama wa nchi hizo na kuandaa uwanja wa makundi ya kigaidi kupata nguvu katika maeneo hayo.
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inatoa muhimu katika siasa zake za nje pia kuhusu ulazima wa kuondoka askari wa kigeni katika eneo na kusisitiza kwamba suluhisho pekee la kufikiwa lengo hilo ni kuboreshwa ushirikiano kati ya nchi za eneo na kutoingilia wageni masuala ya ndani ya nchi za eneo.
Kuendelezwa sera za Iran za kukuza uhusiano na majirani zake kwa lengo la kustawisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi, kumezihimiza nchi za eneo kupanua ushirikiano wao na Iran katika nyuga mbalimbali.
Kufunguliwa tena ubalozi wa Saudi Arabia mjini Tehran kumedhirisha azma mpya ya Iran ya kuboresha kiwango cha ushirikiano wa kieneo na kukaribisha upanuzi wa uhusiano katika nyanja mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni na nchi za eneo hili.
Kutanguliza uhusiano wa kikanda ni jambo zuri la kupunguza uingiliaji wa wageni na kuongeza kasi ya uwekezaji bila ya kuhitaji uwepo wa maslahi binafsi wa makampuni, benki na taasisi za Magharibi, ambazo zinalenga tu kujinufaisha na kupora utajiri wa nchi za Asia Magharibi.
Mpango mwingine muhimu na wa kuvutia wa Iran mara tu baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ulikuwa ni kutetea haki za wananchi wa Palestina jambo ambalo linahesabiwa kuwa moja ya misingi muhimu ya siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Jinai za utawala wa Kizayuni huko Gaza na kutozingatiwa sheria za kimataifa na misingi ya kibinadamu, zimedhihirisha wazi uhalali wa misimamo ya Iran dhidi ya utawala huo bandia kwa nchi za eneo.
Kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni, kutilia maanani zaidi ushirikiano wa kieneo kwa ajili ya kupanua ushirikiano na kukabiliana na Wazayuni kwa kuegemea ushirikiano na majirani ni miongoni mwa vipaumbele vya siasa za nje za Tehran, jambo ambalo leo pia linakaribishwa na nchi za eneo.