Askofu Mkuu wa Azerbaijan, Iran alaani kuvunjiwa heshima Qurani Sweden
Askofu Mkuu wa Kanisa la Armenia katika eneo la Azerbaijan la kaskazini magharibi mwa Iran ameashiria kitendo cha karibuni cha kuchoma moto nakala ya Qur'ani tukufu nchini Sweden na kulaani vitendo hivyo vya kuyavunjia heshima matukufu ya kidini.
Askofu Grigor Chiftchian amesema hayo katika taarifa na kueleza kuwa, uhuru wa maoni na kujieleza haipasi kutafsiriwa kama idhini ya kitendo cha kuvunjia heshima matukufu ya dini nyingine.
Amesema: Ingawaje kitendo hicho kisichokuwa cha kiutu kimefanyika nchini Sweden, lakini kimeungwa mkono na watenda jinai fulani duniani; hatua hii haikubaliki wala kuungwa mkono na wapigania uhuru na haki, na nchi yoyote duniani inayounga mkono amani na usalama.
Askofu Mkuu wa Kanisa la Waarmenia katika eneo la Azerbaijan la kaskazini magharibi mwa Iran amesisitiza kuwa, thamani na matukufu ya kidini lazima yaheshimiwe na hayawezi kufanyiwa dharau na kuvunjiwa heshima kwa namna yoyote ile.
Kiongozi huyo wa Kikristo katika mkoa wa Azerbaijan nchini Iran amesema ameghadhabishwa na kukerwa na vitendo vya kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu huko nchini Sweden.
Huku akitilia mkazo suala la wafuasi wa dini mbalimbali kuishi pamoja kwa amani na maelewano, Askofu huyo wa Waarmenia wa Azerbaijan hapa nchini amepinga vikali misimamo na mitazamo ya kufurutu mipaka.
Katika miezi ya hivi karibuni, nchi za Sweden na Denmark zimeshuhudia hujuma na mashambulizi kadhaa dhidi ya Waislamu na maeneo yao ya kidini, sanjari na kuchomwa moto na kuvunjiwa heshima Kitabu chao kitukufu cha Qur'ani.
Ijumaa iliyopita, mwanamke mmoja mwenye itikadi kali na chuki dhidi ya Uislamu alichoma moto nakala ya Qur'ani Tkufu katika mji wa Malmö nchini Sweden. Kitendo hicho cha kuivunjia heshima Qur'ani Tukufu kilifanywa kwa ulinzi kamili wa polisi wa nchi hiyo na pia usimamizi na uungaji mkono wa jukwaa la Wazayuni.