Maonyesho ya 28 ya Kimataifa ya Mafuta na Gesi ya Tehran
Maonyesho ya 28 ya Kimataifa ya Mafuta, Gesi, Viwanda vya Usafishaji na Petrokemikali ya Iran yalianza Jumatano wiki hii mjini Tehran kwa kushirikisha zaidi ya makampuni 1,500 ya ndani na 250 ya kigeni.
Maonyesho haya yanafanyika katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na makampuni ya sekta zote za mafuta na gesi kuanzia utafutaji, uchimbaji na uzalishaji hadi viwanda vya kusafisha mafuta na petrokemikali. Aidha mashirika mapya ya kiteknolojia yanashiriki katika maonyesho hayo ambayo kaulimbiu yake kuu mwaka huu ni: "Sekta ya Mafuta, Kiwango cha Juu cha Uzalishaji na Uboreshaji wa Teknolojia." Maonyesho hayo yalianza Mei 8 na yanamalizika leo Jumamosi Mei 11.
Maonyesho ya Kimataifa ya Mafuta, Gesi, Viwanda vya Usafishaji na Petrokemikali ya Iran ni tukio kubwa zaidi la aina yake nchini Iran na huwa fursa nzuri kwa kampuni zinazofanya kazi katika tasnia hii kuzindua mafanikio na bidhaa zao kwa washiriki na wataalamu wa kitaifa na kimataifa.
Akizungumza na waandishi wa habari katika maonyesho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Taifa ya Mafuta ya Iran alisema, katika miaka mitatu iliyopita, uzalishaji wa mafuta umeongezeka kati ya asilimia 60 na 70, na zaidi ya akiba ya mapipa bilioni 2.5 ya hidrokaboni mpya (mafuta ghafi na gesi) yaligunduliwa na kuongezwa kwenye akiba ya nchi.
Vilevile mauzo ya Iran ya gesi ya kimiminika (LPG) yameongezeka kwa takriban asilimia 30 katika mwaka uliopita wa Kiirani wa 1402 (uliomalizika Machi 19), ikilinganishwa na takwimu za mwaka uliotangulia wa 1401. Hayo yalitangazwa na kaimu wa Idara ya Masuala ya Kimataifa ya Kampuni ya Gesi ya Iran (NIGC).
Akizungumza kando ya maonyesho hayo siku ya Alhamisi iliyopita, Mohsen Khojastemehr alisema idara yake inaweza kusaidia kuongeza mapato ya fedha za kkigeni kupitia mauzo ya gesi asilia na bidhaa zake.

Mohsen Khojastemehr aliongeza: Mwaka jana, wazalishaji wa ndani walikidhi mahitaji mengi ya sekta ya mafuta, na mapato yaliyotokana na mauzo ya mafuta yalifikia zaidi ya dola bilioni 35.
Waziri wa Mafuta, Javad Oji, akizungumza Jumatano katika hafla ya ufunguzi rasmi wa Maonyesho ya 28 ya Kimataifa ya Mafuta, Gesi, Viwanda vya Usafishaji na Petrokemikali ya Iran, alisema mwaka huu zaidi ya makampuni 1,500 ya ndani na makampuni 250 ya nje yameshiriki katika maonyesho hayo. Alisema maonyesho hayo ni fursa inayofaa kuonyesha mafanikio makubwa ya miaka miwili na nusu iliyopita ya Wizara ya Mafuta katika Serikali ya Awamu ya 13 na kuongeza kuwa: Katika kipindi hiki, uzalishaji wa mafuta ghafi nchini Iran ulikua kwa zaidi ya asilimia 60 kwa kutegemea makampuni ya ndani, na mauzo yake yameongezeka kwa kiwango kikubwa katika kipindi hicho.
Kwa mujibu wa makampuni ya kufuatilia meli, mauzo ya mafuta ya Iran katika soko la kimataifa yameongezeka licha ya vikwazo vya Marekani ambapo mwezi Agosti mwaka jana Kampuni ya Kimataifa ya SVB ilikadiria kuwa uzalishaji wa mafuta nchini Iran mwezi Agosti ulikuwa mapipa milioni 3.15 kwa siku, ambayo ni kiasi kikubwa zaidi tangu 2018.
Mafanikio ya Iran hayakomei tu katika kuongeza uzalishaji na mauzo ya mafuta, bali pia yanaweza kuonekana waziwazi katika sekta zingine za mafuta na gesi. Kufikia Machi mwaka huu, takriban miradi 132 yenye thamani ya dola bilioni 28 na milioni 500 ilikamilika sambamba na kuanzishwa utekelezaji wa miradi 50 yenye thamani ya dola bilioni 47 na milioni 500. Wakati huo huo, zaidi ya dola bilioni 5 za kandarasi zimetiwa saini katika sekta ya gesi nchini Iran.
Mafanikio ya Iran katika kuongeza uzalishaji na uuzaji nje wa mafuta ni kielelezo tosha cha kushindwa kwa vikwazo vya kikatili vya Marekani na kubadilisha vitisho kuwa fursa, jambo ambalo pia limedhihirika vyema katika nyanja kama vile viwanda vya kuzalisha nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani.