Iran: Amani ya Asia Magharibi inategemea kupokonywa silaha Israel
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i111710-iran_amani_ya_asia_magharibi_inategemea_kupokonywa_silaha_israel
Iran inasema kuimaishwa amani kamili na ya kweli, utulivu na usalama katika eneo la Asia Magharibi kunategemea kupokonywa silaha kwa utawala ghasibu wa Israel na kukomeshwa kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina.
(last modified 2024-05-13T03:23:38+00:00 )
May 13, 2024 03:23 UTC
  • Iran: Amani ya Asia Magharibi inategemea kupokonywa silaha Israel

Iran inasema kuimaishwa amani kamili na ya kweli, utulivu na usalama katika eneo la Asia Magharibi kunategemea kupokonywa silaha kwa utawala ghasibu wa Israel na kukomeshwa kukaliwa kwa mabavu ardhi ya Palestina.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir-Abdollahian aliyasema hayo katika hotuba yake kwenye mkutano wa tatu wa Mazungumzo kati ya Iran na Waarabu uliopewa jina la "Kwa Ajili ya Ushirikiano na Maingiliano" uliofanyika jana Jumapili mjini Tehran.

Ameongeza kuwa watu wa Palestina wamenyimwa haki zao zote na "vita visivyo na usawa" vya Israel huko Gaza katika kipindi cha miezi saba iliyopita kwa mara nyingine vimeonyesha ukweli kuhusu suala la Palestina kwa walimwengu.

Amir-Abdollahian ameongeza kuwa, utawala wa Israel uliundwa kwa msingi wa ukiukaji wa haki za Wapalestina, uvamizi, uchochezi wa vita na misimamo mikali na hakuna uwezekano wa utawala huo kuishi pamoja kwa amani na mataifa ya eneo hili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ameilaumu Marekani kwa kuipatia Israel uungaji mkono kamili na usio na masharti katika kutenda jinai na mauaji ya kimbari dhidi ya watu wa Palestina.

Amesisitiza kuwa, Marekani pia imekiuka madai yake yote ya uongo na hadaa ya eti kutetea amani, demokrasia na haki za binadamu.

Amir-Abdollahian amesema amani na utulivu endelevu hautapatikana Palestina na eneo la nchi za Kiarabu na Kiislamu hadi pale watu wa Palestina watakapopata haki zao.

Amesisitiza kuwa mataifa ya Magharibi mwa Asia hususan Wapalestina hawana chaguo ila kuendeleza mapambano kwa ajili ya kupata haki zao kamili.

Zaidi ya Wapalestina 35,000, wengi wao wakiwa ni watoto na wanawake, wameuawa katika vita vilivyoanzishwa na Israel tarehe 7 Oktoba 2023 kufuatia operesheni ya kulipiza kisasi ya harakati za mapambano ya ukombozi za Palestina.