Azma ya Iran ya kuimarisha ushirikiano na nchi za kieneo
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i111716-azma_ya_iran_ya_kuimarisha_ushirikiano_na_nchi_za_kieneo
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir Abdollahian amesisitiza katika kikao cha mkutano wa tatu wa Mazungumzo kati ya Iran na Waarabu uliopewa jina la "Kwa Ajili ya Ushirikiano na Maingiliano" kwamba Iran imeazimia kukuza na kuzidisha maelewano na ushirikiano na nchi za eneo la Magharibi mwa Asia.
(last modified 2024-05-13T08:04:11+00:00 )
May 13, 2024 08:04 UTC
  • Azma ya Iran ya kuimarisha ushirikiano na nchi za kieneo

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Hossein Amir Abdollahian amesisitiza katika kikao cha mkutano wa tatu wa Mazungumzo kati ya Iran na Waarabu uliopewa jina la "Kwa Ajili ya Ushirikiano na Maingiliano" kwamba Iran imeazimia kukuza na kuzidisha maelewano na ushirikiano na nchi za eneo la Magharibi mwa Asia.

Mkutano wa Mazungumzo kati ya Iran na Waarabu uliopewa jina la "Kwa Ajili ya Ushirikiano na Maingiliano" ulifanyika jana Jumapili, Mei 13, kwa hotuba ya Hossein Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje, ukihudhuriwa na wanafikra na shakhsia wa kisiasa. Mkutano huo uliandaliwa na Baraza la Kistratijia la Mahusiano ya Kigeni mjini Tehran.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran amesema katika mkutano huo kwamba, kwa kuzingatia sera ya ujirani, Iran imefanya juhudi za ustawi wa pamoja na majirani zake wote, Ulimwengu wa Kiislamu na Ulimwengu wa Kiarabu, na mfano wa wazi wa jambo hilo ni jitihada za kurejea uhusiano wa kawaida kati ya Riyadh na Tehran. 

Baadhi ya washiriki katika mkutano wa Iran na Waarabu

Kuhusu mpango wa Iran kwa ajili ya Palestina, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliwasilisha mpango wa kura ya maoni ya kidemokrasia miaka kadhaa iliyopita na kuusajili katika Umoja wa Mataifa kama suluhisho la kisiasa la mgogoro huo, na suala la Palestina linapaswa kuwa kitovu cha masuala yanayopewa uzito cha Ulimwengu wa Kiislamu.

Hossein Amir Abdollahian

Katika miaka ya hivi karibuni, maafisa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima wamekuwa wakitilia mkazo suala la kutoa kipaumbele kwa uhusiano mwema na majirani katika sera za kigeni za Jamhuri ya Kiislamu. Iran imekuwa na nafasi muhimu na madhubuti katika kuimarisha amani na usalama katika eneo la Magharibi mwa Asia, na uwepo wa vikosi vya jeshi la nchi hii katikka maeneo muhimu, kwa namna fulani, umetuliza na kupunguza mivutano. Nafasi ya vyombo vya usalama na jeshi la Iran imekuwa na ufanisi mkubwa katika kukabiliana na harakati za makundi ya kigaidi, na makundi hayo na waungaji mkono wao wa nchi za Magharibi, yameshindwa kuendeleza njama na kuzusha mivutano na ukosefu wa usalama katika eneo hili. 

Marekani na nchi za Ulaya zinazoiunga mkono Ikulu ya White House, katika miaka ya hivi karibuni zimechangia pakubwa katika kuendeleza ukosefu wa amani na utulivu katika eneo la Magharibi mwa Asia kwa kuyaunga mkono makundi ya kigaidi, na kuwepo  jeshi la Marekani nchini Iraq, Afghanistan na Syria kumezidisha ukosefu wa usalama katika maeneo hayo na kutayarisha mazingira ya kujiimarisha vikundi vya kigaidi.

Katika mtazamo wake wa siasa za nje pia, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inasisitiza ulazima wa kuondoka askari wa kigeni katika eneo hili na inaona kwamba, suluhisho pekee la matatizo yaliyopo ni ushirikiano wa nchi za kanda na hakikisha kwamba madola ya kigeni hayaingilii masuala ya ndani ya nchi nchi za kanda hiyo.

Mkutano wa Iran na Waarabu

Kuendelea sera hizi za Iran za kuimarisha ushirikiano na majirani zake kwa lengo la kuzidisha uhusiano wa kisiasa na kiuchumi, kumezihamasisha nchi za eneo hili kupanua ushirikiano na Iran katika nyuga mbalimbali. Kufunguliwa tena ubalozi wa Saudi Arabia mjini Tehran kunaonyesha mwelekeo mpya wa Iran wa kuzidisha ushirikiano wa kikanda na kupanua uhusiano katika nyuga mbalimbali za kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni.

Mwelekeo mwingine muhimu wa Iran baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ni kutetea haki za watu wa Palestina, jambo ambalo linahesabiwa kuwa moja ya mihimili muhimu ya siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Jinai zinazofanywa na utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza na kukanyaga kake sheria za kimataifa na misingi ya kibinadamu, vimedhihirisha wazi usahihi wa misimamo ya Iran dhidi ya utawala huo bandia kwa nchi za eneo la Asia Magharibi na ulimwengu mzima kwa ujumla. Suala hili limechochea zaidi hamu ya kuimarisha zaidi uhusiano wa kikanda na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.