Sera za Iran kuhusu nishati ya nyuklia hazijabadilika
Nasser Kanani, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alitangaza Jumatatu 13 Mei kwamba, sera za nyuklia za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hazijabadilika.
Suala la nyuklia ni mojawapo ya masuala ambayo yamepewa kipaumbele muhimu katika sera za kigeni za Iran katika miongo miwili iliyopita. Hii ni katika hali ambayo maadui wamejaribu kuituhumu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa inataka kuunda silaha za nyuklia, tuhuma ambazo zimekuwa zikikanushwa mara kwa mara na viongozi wa Iran ambao wakisisitiza kuwa mpango wa nyuklia wa Iran ni wa malengo ya amani. Ayatullah Khamenei, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran pia amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu, ni haramu kumiliki silaha za nyuklia. Amesema kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inaamini kuwa utumiaji wa silaha za nyuklia, za kemikali na nyinginezo za maangamizi ya umati ni dhambi kubwa na isiyosameheka. Kiongozi wa Mapinduzi pia alisema sehemu nyingine: "Hatukubali silaha za nyuklia si kwa sababu ya Marekani na wasiokuwa Marekani, bali kwa sababu ya imani yetu; hakuna mtu anayepaswa kuwa na silaha hizo. Tunaposema msiwe na silaha hizo maana yake ni kuwa sisi pia hatupaswi kuwa nazo na hatutakuwa nazo."
Suala la uwezekano wa Iran kutazama upya mpango wake wa nyuklia limekuwa likijadiliwa na pande mbalimbali katika siku za karibuni. Kwanza, Kamal Kharazi, Mkuu wa Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Iran akijibu swali katika mahojiano na "Al-Jazeera Mubashar" kuhusu tishio la utawala wa Kizayuni kushambulia kituo cha nyuklia cha Isfahan alisisitiza kuwa, iwapo Iran itatishiwa, basi italazimika kubadilisha sera zeke za kujilinda. Alisema ”…Ikiwa watapata ujasiri wa kutaka kudhuru taasisi zetu za nyuklia, basi kiwango chetu cha kuzuia hujuma ya maadui kitabadilika. Kufikia sasa tumepatia uzoefu tofauti wa viwango hivyo, hivyo iwapo watavamia vituo vyetu vya nyuklia, hatua hiyo inaweza kupelekea kutazamwa upya sera za nyuklia za Iran." Matamshi hayo ya Kharazi yalikabiliwa na radiamali nyingi ambapo kwa mara nyingine tena siasa za chuki na propaganda dhidi ya Iran zimefanywa kuwa ajenda kuu ya vyombo vya habari na serikali za Magharibi, hasa Marekani. Huku, akisisitiza kwamba sera za nyuklia za Iran hazijabadilika, Nasser Kanani Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran amesema kuhusu onyo la Kharazi juu ya uwezekano wa kutazamwa upya sera za nyuklia za Iran kuwa: Iran imekuwa ikisisitiza na kuweka wazi msimamo wake wa kupinga uzalishaji na usambazaji wa silaha za maangamizi ya umati na kwa mujibu wa fatwa ya wazi ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Kwa msingi huo, imepasisha mikataba ya kimataifa inayozuia silaha za mauaji ya halaiki na kutia saini mikataba ya kupiga marufuku majaribio yote ya silaha za nyuklia. Kuwepo silaha za nyuklia kunatishia amani na jamii ya mwanadamu duniani. Pia, Iran imekuwa na bado inasisitiza juu kuheshimiwa na kutekelezwa kikamilifu Mkataba wa Kuzuia Silaha za Nyuklia. Ukweli ni kwamba kilichomchochea Mkuu wa Baraza la Mahusiano ya Kigeni la Iran kutoa maoni aliyotoa ni vitisho vya mara kwa mara vya utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran na hasa vya kutaka kulenga vituo vyake vya kijeshi. Kwa hakika, vitisho kama hivyo vinaweza kuifanya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itazame upya sera zake za nyuklia. Matamshi ya Kamal Kharrazi ni onyo pia kwa utawala wa Kizayuni na wala hayahesabiwi kuwa ni ishara ya kubadilika sera za Iran kuhusu mpango wake wa nyuklia.