May 20, 2024 11:50 UTC
  • Rambirambi za Kiongozi Muadhamu kufuatia kufa shahidi Rais Raisi na wenzake

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametoa salamu za rambirambi kufuatia kufa shahidi Seyed Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na ujumbe alioandamana nao.

Kwa mujibu wa tovuti ya kituo cha habari cha Ofisi ya Kiongozi Muadhamu, Ayatullah Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe wake leo Jumatatu, ametuma salamu za rambi rambi kufuatia kufa shahidi katika ajali ya helikopta jana Seyyed Ebrahim Raisi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya  Iran, Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje,  Hujjatul Islam wal Muslimin Al Hashem, mwakilishi wa Waliul Faqih katika Mkoa wa Azabajan Mashariki, Malik Rahmati, Gavana wa Azabajani Mashariki na wote waliokuwa katika msafaraha huo.

Kiongozi Muadhamu amesema: "Nimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa chungu za kufa shahidi mwanachuoni Mujahid, rais hodari na mchapakazi, mhudumu wa Imam Ridha (AS), Hujjatul Islam wa Muslimin, Sayyid Ibrahim Raisi na alioandamana nao; Mwenyezi Mungu awarehemu."

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameendelea kusema kuwa, tukio hili la kusikitisha limetokea wakati Rais Raisi alikuwa katika jitihada kubwa za kuwahudumia wananchi. Ameongeza kuwa: "Katika kipindi chote cha huduma na kujitolea, katika kipindi kifupi cha urais na kabla ya hapo, alijitihadi bila kikomo katika kuwatumikia wananchi, nchi na Uislamu.

Ayatullah Khamenei ameashiria kwamba Rais Raisi hakujua uchovu na katika tukio hili chungu, taifa la Iran limempoteza mtumishi mwaminifu, mkweli na mwenye thamani kubwa. Amesema Raisi alitanguliza ustawi wa nchi na wananchi, ambao ni kwa ajili ya kumridhisha Mwenyezi Mungu, kuliko kila kitu na kwa hiyo kero za waovu na dhihaka za baadhi ya watu wasiofaa hazikumzuia kufanya kazi usiku na mchana ili kuboresha na kurekebisha mambo nchini.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema; Katika tukio hili zito, watu mashuhuri kama vile Hujjatul Islam Al Hashem, Imam maarufu na anayeheshimika wa Ijumaa wa Tabriz, Hossein Amir Abdullahian,  Waziri wa Mambo ya Nje ambaye alikuwa mujahid na mwanaharakati, Malik Rahmati, gavana mwanamapinduzi na mcha Mungu wa Azerbaijan Mashariki, marubani na wengine katika msafara huo nao pia wamekumbatia rehema ya Mwenyezi Mungu.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameongeza kuwa: "Natangaza siku tano za maombolezo ya umma na kutoa pole kwa taifa adhimu la Iran."

Aidha amesema kwa mujibu wa Ibara ya 131 ya Katiba, Mohammad Mokhbir, (ambaye sasa ni makamu wa kwanza wa rais) atakaimu nafasi ya utendaji ya rais na pia atakuwa na jukumu la kusimamia serikali na kushirikiana na spika wa bunge na mkuu wa idara ya mahakama ili katika kipindi cha siku hamsini zijazo uchaguzi wa rais mpya ufanyike.