Mahudhurio makubwa ya kuwaaga Mashahidi Wahudumu wa Iran
Mahudhurio makubwa ya wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika hafla ya mazishi ya shahidi Ebrahim Raisi na wenzake ambao walikufa shahidi katika ajali ya helikopta katika eneo la milimani la mkoa wa Azarbaijan Mashariki, kaskazini-magharibi mwa Iran kwa mara nyingine tena yamedhihirisha mshikamano na umoja wa taifa la Iran na nia yao ya kuendeleza njia ya mapambano na muqawama.
Siku ya Jumatano tarehe 22, 2024 mamilioni ya watu walishiriki katika mazishi ya kuwaaga mashahidi Rais Sayyid Ebrahim Raisi, Hussein Amir Abdollahian Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na mashahidi wenzao wengine mjini Tehran.
Mazishi hayo yalianza saa 7:30 asubuhi katika Chuo Kikuu cha Tehran, na ilipotimia saa 9:00 asubuhi, Ayatulla Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran akawa amewasili na kuongoza swala ya kuswalia miili ya mashahidi hao na baada ya hapo, miili ikatolewa katika Msikiti wa Chuo Kikuu cha Tehran hadi uwanja wa Mnara wa Azadi.
Mbali na wakazi wa Tehran, baadhi ya waombolezaji kutoka miji na mikoa mingine walikuwa wamefika katika Chuo Kikuu cha Tehran siku moja kabla kwa ajili ya kushiriki katika swala na mazishi ya mashahidi hao watukufu, ambapo wengi walibeba picha ya Shahid Raisi na bendera ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Mahudhurio makubwa ya watu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika mazishi ya mashahidi hao ni ukumbusho wa anga iliyotawala katika miji ya Iran katika mazishi ya mashahidi wengine wa zamani Rajaee na Bahonar mnamo mwaka 1981.
Pia yanakumbusha mazishi ya kamanda kipenzi wa wananchi wa Iran na watu wengine wengi duniani, mjini Tehran Shahidi Luteni Haj Qassim Suleimani, Kamanda wa Kikosi cha Quds cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC), aliyeuawa kigaidi na Wamarekani akiwa safarini nchini Iraq Januari 3, 2020.
Hayo yanajiri licha ya kwamba maadui daima wanajaribu kuleta hitilafu na mgawanyiko baina ya wananchi na viongozi wa mfumo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Maadui wamejaribu mara nyingi kulenga mshikamano na umoja wa wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu kwa kuibua baadhi ya matatizo na hitilafu bandia katika masuala ya nchi, na hivi sasa mahudhurio ya mamilioni ya watu katika mazishi hayo ya mashahidi Sayyid Raisi na wenzake yameonyesha mshikamano mkubwa uliopo kati ya raia wa Iran viongozi wao, jambo ambalo linathibitisha wazi kwamba watu wenye nia mbaya, yaani maadui wa Iran siku zote wanakosea katika kuwatambua Wairani.
Nukta nyingine muhimu ni mahudhurio ya viongozi wa nchi za kigeni katika mazishi ya viongozi shahidi wa Iran, jambo ambalo bila shaka linaakisi hadhi na itibari ya kimataifa ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Takriban viongozi 15 na maafisa wakuu wa nchi 13 waliwasili mjini Tehran kuhudhuria hafla za kutoa heshima zao za mwisho kwa mwili wa Sayyid Raisi na wenzake waliokufa shahidi katika ajali ya helikopta nchini Iran.
Tamim bin Hamad Al-Thani Amir wa Qatar, kiongozi wa kitaifa wa Turkmenistan, marais wa Tunisia na Tajikistan, mawaziri wakuu wa Iraq, Pakistan, Armenia, Qatar, Azerbaijan na maspika wa mabunge ya Iraq, Russia, Algeria, Uzbekistan, Kazakhstan na Lebanon ni miongoni mwa viongozi hao walifika mjini Tehran kwa ajili ya shughuli hiyo, ambapo baadhi yao waliweza kupata fursa ya kukutana na Ayatullah Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Ni wazi kuwa mahudhurio makubwa ya wananchi na viongozi wa kigeni katika mazishi ya mashahidi wa ajali ya helikopta iliyombeba Shahid Rais Ebrahim Raisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran pamoja na ujumbe wa ngazi za juu alioandamana nao yanapaswa kuzingatiwa kama dhihirisho la shukrani za taifa la Iran kwa watumishi wake waaminifu na pia dhihirisho jingine la utukufu wa taifa la Iran.
Mahudhurio hayo makubwa pia yamethibitisha kwa mara nyingine kwamba wananchi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima wanaheshimu na kuwaenzi viongozi wao ambao wamejaribu kwa dhati kuwa watiifu na waaminifu kwa malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu, Kiongozi Muadhamu na njia ya mashahidi.