May 25, 2024 08:07 UTC
  • Putin: Misingi ya serikali ya Iran ni madhubuti na imara

Ikiwa ni katika kuzungumzia kufa shahidi Rais Ebrahim Raisi wa Iran na wenzake katika ajali ya helikopta iliyotokea huko kaskazini magharibi mwa nchi , Rais wa Russia amesema, hatarajii mabadiliko yoyote kutokea katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa sababu misingi ya serikali ya Iran ni thabiti na imara.

Rais Vladmir Putin wa Russia amesema ana imani kuwa Tehran itaendelea na mkondo wake wa sasa katika siasa za nje baada ya kifo cha shahidi Ebrahim Raisi na kusema: “Baada ya tukio hili la kuhuzunisha, hatuwezi kutarajia mabadiliko katika siasa za nje za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa sababu mihimili ya serikali ya Iran ni imara, yenye nguvu na yenye kutegemewa ulimwenguni kote.

Rais Putin, akijibu swali la mwandishi wa habari baada ya kumalizika mazungumzo kati ya Russia na Belarus amesema kuwa, siasa za mambo ya nje ya Jamhuri za Kiislamu ya Iran zinatokana na kujitawala nchi hii na kuongeza kuwa Iran ni nchi kubwa ya kieneo ambayo ina nafasi kubwa katika masuala ya kimataifa.

Siku nne zilizopita, Ikulu ya Kremlin ilitoa salamu za rambirambi kufuatia kufa shahidi hayati Ebrahim Raisi, Waziri wa Mambo ya Nje Hussein Amir-Abdollahian na wenzake aliokuwa amefuatana nao katika safari hiyo.

Rais wa Russia pia amesema katika mazungumzo ya simu na kaimu Rais wa Iran Mohammad Mokhber kwamba Moscow imejitolea kuendelea kuimarisha ushirikiano wa pande zote na Tehran. Amesema Russia alimwona marehemu Rais kuwa mshirika wa kuaminika kwa sababu alichangia pakubwa katika kustawisha uhusiano wa Russia na Iran.

 

Tags