Persepolis yatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Iran
(last modified Sun, 02 Jun 2024 10:29:43 GMT )
Jun 02, 2024 10:29 UTC
  • Persepolis yatwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka Iran

Klabu ya Persepolis ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imetwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Soka hapa nchini baada ya kuichachafya klabu ya Mes Rafsanjan Jumamosi. Esteqlal imemaliza ya pili baada ya kuisasambua Peykan mabao 2-0.

Katika kipute hicho cha kukata na shoka, vijana wa Persepolis au ukipenda waite Wekundu wa Tehran waliwabamiza Mes Rafsanjan bao 1-0 katika mchezo uliopigwa katika Uwanja wa Azadi hapa jijini Tehran.

The Reds walianza kwa kasi nzuri na kutawala mchezo huo, huku beki raia wa Georgia, Giorgi Gvelesiani akifunga bao hilo la kipekee na la ushindi kunako dakika ya 86 ya mchezo, na kuifanya timu hiyo ifikishe jumla ya alama 68, pointi moja zaidi ya Esteqlal ambayo imefunga msimu kwa alama 67.

Wekundu wa Tehran walipoteza fursa nyingi za wazi kabla ya kumalizika kipindi cha kwanza huku shuti za washambuliaji wake zikikosa kutikisa nyavu. 

Vijana wa Persepolis wakiusakata kabumbu

Hii ni mara ya tisa kwa Persepolis kushinda ligi. Klabu hiyo ya kandanda ya Iran ilishinda taji hili kwa mara ya kwanza katika msimu wa ligi ya mwaka 2001-2002.

Klabu ya Sepahan ni katika timu ambazo zimetwaa Ligi Kuu ya Soka ya Iran inayofahamika pia kama Persian Gulf Pro League mara nyingi zaidi, ikizingatiwa kuwa imetwaa taji hilo mara tano; katika misimu ya mwaka 2002-03, 2009-10, 2010-11, 2011-12 and 2014-15.