Bagheri Kani katika mkondo wa diplomasia ya muqawama
Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika muendelezo wa safari yake ya kieneo jana aliwasili Damascus, mji mkuu wa Syria kwa minajili ya kukutana na kufanya mashauriano na viongozi wa serikali ya nchi hiyo ya Kiarabu.
Mkutano huo ulifanyika katika ubalozi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran mjini Damascus kwa kuhudhuriwa na balozi wa Iran.
Mwanzoni mwa safari yake ya kieneo, Ali Bagheri Kani alisema kuwa, kuongezeka ushirikiano wa harakati za Mapambano ya Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni kwamba, ni moja ya malengo makuu ya safari yake ya kieneo.
Hiyo ilikuwa ni safari yake ya kwanza ya kikanda kwa Ali Bagheri Kani tangu alipochukua wadhifa wa Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Majadiliano kuhusiana na kuongezwa ushirikiano na uhusiano kati ya Tehran na Damascus, mgogoro wa Ukanda wa Gaza na ulazima wa kukomeshwa jinai za utawala wa Kizayuni dhidi ya wananchi wa Palestina ni miongoni mwa ajenda kuu za mazungumzo kati ya pande hizo mbili.
Kabla ya kuondoka kuelekea Damascus, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, alikutana na kuzungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Lebanon Abdullah Bou Habib, Waziri Mkuu wa nchi hiyo Najib Miqati, Spika wa Bunge Nabih Berri, na Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon.
Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alizuru pia Raudhat-al-Shuhadaa na kutoa heshima zake kwa mashahidi wa Muqawama wa Kiislamu wa Lebanon waliozikwa katika eneo hilo kama ambavyo alizuru kaburi la mama yake Sayyid Hassan Nasrullah, Katibu Mkuu wa Hizbullah, na akawasomea Fatiha.
Vyombo vya habari vya Lebanon vilitangaza habari ya kukutana kwa Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran na Katibu Mkuu wa Hizbullah ya Lebanon Sayyid Hassan Nasrullah mjini Beirut na kuandika kuwa, pande hizo mbili zimejadili matukio ya hivi karibuni zaidi ya kisiasa na kiusalama katika eneo hususan katika kambi ya Gaza na Lebanon.
Kwa ujumla katika ziara yake, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Iran huko Lebanon na Syria ambayo mbali na kukutana na kufanya mazungumzo na maafisa rasmi wa nchi hizo iliambatana na kukutana na viongozi wa muqawama wa Palestina na Lebanon ni muhimu na ina jumbe kadhaa:
Kwanza kabisa inaonyesha kwamba, licha ya kuwa, pengo la nafasi ya marehemu Amir Abdollahian, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya awamu ya 13, na mashahidi wengine waliopata ajali ya anga, bado linashuhudiwa katika idara ya sera za kigeni na za ndani za Iran, lakini urithi wake aliouacha katika idara ya kigeni, iwe ni katika kuimarisha kiunganishi cha mawasiliano cha uga wa diplomasia au iwe ni katika muktadha wa kufuata sera ya "majirani wa kwanza" au mambo mengine ungalipo na utaendelea kwa nguvu zote kimantiki na katika fremu iliyoainishwa na Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Nukta ya pili ni kuwa, kukabiliana na jinai za utawala wa Kizayuni wa Israel huko Gaza ni katika vipaumbele vya siasa za kigeni wa Iran. Katika uwanja huo na kama ilivyoshuhudiwa katika safari ya Bagheri Kani ni kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inafanya juhudi za kutumiwa uwezo wa mhimili wa muqawama na ulimwengu wa Kiislamu kwa ajili ya kufikia lengo hilo. Ni kwa kuzingatia ukweli huo ndio maana Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imependekeza kufanyika kikao cha dharura cha Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC). Kikao hicho hata kama hakitafanikiwa kusitisha vita vya Gaza lakini kitasaidia kupunguza machungu na mateso wanayoyapata watu wa ukanda wa Gaza ambao wanakabiliwa na holocaust ya kweli.