Jun 14, 2024 10:22 UTC
  • Uchaguzi wa rais Iran: Qalibaf aongoza katika utafiti wa maoni

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran), Mohammad Baqer Qalibaf anaongoza katika utafiti wa maoni, kuelekea uchaguzi wa mapema wa rais unaotazamiwa kufanyika Juni 28.

Matokeo ya uchunguzi wa maoni uliofanywa na taasisi ya 'Poll of Polls' na kuchapishwa na tovuti ya Press TV yanaonesha kuwa, Qalibaf yuko kifua mbele kwa asilimia 22.

Utafiti huo uliofanywa na taasisi huru unaonesha kuwa, Saeid Jalili ambaye ni mjumbe mkuu wa zamani wa mazungumzo ya nyuklia ya Iran anashika nafasi ya pili kwa asilimia 19.2, akifuatiwa na mbunge mwandamizi Masoud Pezeshkian, ambaye amewahi kuwa Waziri wa Afya, ambaye ameambulia asilimia 9.8.

Utafiti huo ulifanyika baina ya Juni 11 na 13, na kuwashirikisha Wairani waliotimiza masharti na vigezo vya kupiga kura hapa Tehran na katika mikoa mingine kadhaa ya nchi.

Mwanasiasa mkongwe, Saeid Jalili aliyeshika nafasi ya pili katika utafiti wa maoni

Uchunguzi huo wa maoni unaonyesha kuwa, asilimia 41 ya wapigakura hawajaamua watampigia nani kura.

Wagombea sita akiwemo Jalili na Qalibaf wameidhinishwa na Baraza la Kulinda Katiba kuwania urais katika uchaguzi wa rais wa kabla ya wakati uliopangwa kufanyika Juni 28.

Kura hiyo iliitishwa baada ya Rais Ebrahim Raisi kufa shahidi katika ajali ya helikopta akiwa na watu wengine saba mnamo Mei 19, katika mkoa wa Azerbaija Mashariki, kaskazini-magharibi mwa Iran.

 

 

 

Tags