Jun 22, 2024 02:26 UTC
  • Jibu la Iran kwa shutuma zisizo na msingi za Marekani kuhusu Yemen

Balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa amezitaja tuhuma za Marekani dhidi ya Iran kuhusu Yemen kuwa, hazina msingi wowote na kusema kwamba, Jamhuri ya Kiislamu daima imekuwa ikitilia mkazo utatuzi wa amani wa mgogoro wa Yemen kupitia njia za kidiplomasia.

Amir Saeid Iravani, amesema hayo katika barua yake kwa mwenyekiti wa muda wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa na kusisitiza kuwa, madai yaliyotolewa na mwakilishi wa Marekani dhidi ya Iran katika mkutano wa wazi wa baraza hilo, hayana msingi wowote. Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa liliitisha kikao Juni 13, 2024 kujadili hali ya Yemen.

Katika barua yake hiyo, Balozi Iravani amesema, kwa bahati mbaya, mwakilishi wa Marekani ametumia vibaya jukwaa la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kama kawaida ya Washington, kutoa tuhuma dhidi ya nchi huru bila ya ushahidi wowote.

Ukweli wa mambo ni kwamba, Marekanii ina wasiwasi sana na misimamo huru ya nchi kama Iran, Russia China na Brazil.

Marekani kwa upande mmoja inafanya njama kwa kila njia kuyabambikizia kesi mataifa hayo katika vikao na majukwaa ya kimataifa kwa kutoa tuhuma za uwongo kabiisa, na wakati huo huo kuzuia kuweko umoja na kuimarisha ushirikiano miongoni mwao mwa mataifa hayo.

Makombora ya wanamuqawama wa Yemen

 

Mohsen Rui Sefat, mtaalamu wa masuala ya kisiasa, anasema kuhusu hili: Hivi karibuni Marekani na Uingereza zimeshadidisha hujuma zao dhidi ya Yemen kwa kukiuka kanuni zote za kimataifa na zinadhani kwamba kwa mashambulizi hayo zitaweza kusambaratisha muqawama wa watu wa Yemen. Katika hali hii Marekani inafanya kila iwezalo kuhalalisha jinai zake huko Yemen kupitia kuituhumu Iran.

Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Amir Saeid Iravani, amesisitiza kuwa, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inakanusha vikali tuhuma zisizo na msingi za Marekani dhidi yake na kwamba mara kadhaa Tehran imetangaza kwamba inaheshimu kikamilifu maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya Yemen na haiingilii masuala ya ndani ya nchi hiyo bali dhamira yake kuu ni kuhakikisha mgogoro wa Yemen unatatuliwa kidiplomasia na kwa njia za amani.

Wakati huo huo, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikieleza dhamira yake ya kuheshimu usalama wa baharini na uhuru wa usafiri wa majini, na kwa hakika, Iran ni moja ya nguzo za kudhaminii utulivu wa usalama wa baharini.

Ukweli ni kwamba, Marekani na washirika wa muungano wake wanafanya vitendo vya uchokozi dhidi ya mamlaka ya ardhi ya Yemen kwa visingizio mbalimbali, ambavyo vinakiuka pakubwa sheria za kimataifa, ambapo matokeo ya hilo ni kuhatarisha amani na usalama wa eneo na kukwamisha juhudi za kufikia suluhisho la amani nchini Yemen.

Abdul-Malik al-Houthi, Kiongozi wa Ansarullah ya Yemen

 

Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kuwa, uvamizi wa Marekani na Uingereza huko Yemen unazidisha mgogoro wa kibinadamu wa nchi hiyo masikini ya Kiarabu. Kwa hiyo, Marekani haiwezi kukana wajibu wake katika suala hili kwa kutoa shutuma za uongo dhidi ya nchi nyingine. Kwa hakika huu ni mchezo wa kuigiza wa Marekani na washirika wake ambao wamekuwa wakiukariri mara kwa mara.

Alaa kulli haal, mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa katika barua yake kwa mwenyekiti wa muda wa Baraza la Usalama na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine amesisitiza kuwa, matumizi ya mbinu zilizofeli kama vile kusema uwongo na kampeni ya kueneza uwongo kuhusu hali ya Yemen inayotumiwa na Marekani kuhalalisha hujuma na uvamizi wa Washington dhidi ya uhuru na mamlaka ya kujitawala ardhi ya Yemen.

Kwa muktadha huo, tuhuma za uongo za Marekani dhidi ya Iran ni kifuniko tu cha kuendeleza maovu na jinai za Marekani, Uingereza na waitifaki wao wengine huko Yemen, jambo ambalo linafanya maisha ya watu wa nchi hiyo kuwa magumu zaidi hususan watoto na wanawake.