Jun 22, 2024 06:52 UTC
  • Uchunguzi wa maoni: Jalili anaongoza katika mbio za uchaguzi wa rais Iran

Ikiwa imesalia wiki moja tu kabla ya uchaguzi wa rais wa mapema uliopangwa kufanyika Juni 28 katika Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, wapiga kura hapa nchini wangali wanapanga na kupangua kuhusu nani watamchagua kushika hatamu za kuongoza serikali ya Awamu ya 14 ya Jamhuri ya Kiislamu.

Matokeo ya karibuni ya uuchunguzi wa maoni yanaonyesha kuwa, Saeed Jalili, mwanasiasa mkongwe ambaye aliwahi kuwa mkuu wa Usalama wa Taifa na pia kiongozi ya timu ya Iran katika mazungumzo ya nyuklia na mataifa ya Magharibi, anawatimulia kivumbi wagombea wengine.

Uchuguzi huo wa maoni uliotolewa jana Ijumaa unaonyesha kuwa, Jalili anaongoza na amewaacha nyuma wapinzani wake wangine watano katika mbio za kuwania kiti cha rais wa Iran. 

Matokeo ya uchunguzi huo wa maoni uliofanywa na vyombo vya kujitegemea yanaonyesha kuwa, kutakuwepo mchuano mkali kati ya Saeed Jalili, Spika wa Bunge Mohammad Baqer Qalibaf, na mbunge Masoud Pezeshkian, na kwamba kuna uwezekano wa uchaguzi kuingia duru ya pili ya upigaji kura.

Utafiti mwingine wa maoni unaonyesha kuwa, Pezeshkian kwa sasa yuko mbele ya Jalili na Qalibaf. Utafiti huo uliofanyika Juni 18, 19, na 20, ulijumuisha wahojiwa kutoka Tehran, na maeneo mengine kadhaa ya vijiji vilivyochaguliwa.

Katika sehemu ya kwanza ya utafiti huo, asilimia 22.5 ya washiriki katika uchuguzi huo wa maoni amesema watampigia kura Jalili.

Qalibaf, spika wa bunge mara mbili na mbunge mkongwe, anashika nafasi ya tatu kwa kupata asilimia 19.5 ya kura. Pezeshkian anafuatia kwa karibu akiwa na asilimia 19.4.

Wagombea sita wanaowania kiti cha uraisi wa Jamhuri ya Kiislamu, walioidhinishwa na chombo cha juu cha kusimamia uchaguzi nchini, kwa sasa wanafanya kampeni na midahalo ya kisiasa ya kutangaza sera zao.

Uchaguzi wa rais wa mapema wa Iran ulioitishwa baada ya kifo cha rais Sayyid Ebrahim Raisi aliyeaga dunia kwa ajali ya helikopta Mei 19, 2024,  utafanyika Juni 28 ndani ya nchi na katika vituo maalumu vya kupigia kura katika nchi mbalimbali kwa Wairani wanaoishi nje ya nchi.