Jun 23, 2024 11:13 UTC
  • Mgombea Urais: Iran haipaswi kujifunga katika mazungumzo na nchi chache tu

Saeed Jalili, mgombea wa urais wa Iran unaotarajiwa kufanyika Ijumaa ya wiki hii ya Juni 28, amesema kuwa, Iran haipaswi kujifunga katika mazungumzo na nchi chache tu, bali inabidi kuwa wazi kwa nchi zote duniani.

Amesema hayo katika kampeni za uchaguzi alizofanywa katika Chuo Kikuu cha Teknolojia cha Sharif hapa mjini Tehran jana Jumamosi. Amesema hayo kugusia mazungumzo ya kufufua makubaliano ya nyuklia ya JCPOA ambayo Marekani ilitia ulimi puani na kukataa kuyatekeleza.

Jalili, ambaye wakati fulani aliongoza timu ya Iran ya mazungumzo ya nyuklia ni mkosoaji mkubwa wa mapatano ya JCPOA.

Amesema kuwa, kilichoandikwa katika mapatano ya JCPOA ni tofauti na kinachozungumzwa katika kusifia mapatano hayo.

Katika kuuthibitishia ulimwengu kivitendo kuwa mradi wake wa nyuklia ni wa amani kikamilifu, Iran ilifikia makubaliano ya JCPOA na baadhi ya madola yenye nguvu duniani yaliyoanza kutekelezwa mwaka 2015. Hata hivyo, mwezi Mei 2018 Marekani ilikanyaga makubaliano hayo ikatia ulimi pua, ikajitoa na kuirejeshea Iran vikwazo vyote vilivyokuwa vimeondolewa baada ya kufikiwa mapatano hayo. 

Mazungumzo ya kufufua makubaliano hayo yalianza katika mji mkuu wa Austria, Vienna mwezi Aprili 2021, kwa nia ya kuondoa vikwazo dhidi ya Iran na kuishinikiza Marekani kurudi katika mapatano hayo.

Lakini mazungumzo hayo ya Vienna, yamesimama tangu mwezi Agosti 2022 kutokana na msisitizo wa Washington wa kukataa kuondoa vikwazo vyote na kushindwa kutoa hakikisho linalotakiwa kwamba haitojitoa tena katika JCPOA.