Jun 26, 2024 02:17 UTC
  • Tehran, mwenyeji wa Jumuiya ya Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia (ACD).

Kikao cha 19 cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia (ACD) kilifanyika Jumatatu hapa mjini Tehran chini ya uenyekiti wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Akizungumza katika hafla ya ufunguzi wa kikao hicho, Ali Bagheri Kani, Kaimu Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alifafanua siasa za Tehran katika kuimarisha ushirikiano wa kieneo na kimataifa, na kusema kikao cha Tehran mbali na kuimarisha ushirikiano kati ya nchi za Asia, pia kinaonyesha hamu ya nchi hizo ya kuboresha ushirikiano wa pande kadhaa. Bagheri ameongeza kuwa Iran inajivunia kuwakaribisha wawakilishi wa jumbe 41 za Jumuiya ya Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia mjini Tehran na kwamba inachukua hatua za kivitendo na madhubuti kwa ajili ya kuimarisha shughuli za jumuiya hiyo.

Jumuiya ya Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia ilianzishwa Juni 2002 kwa lengo la kuimarisha ushirikiano na maelewano kati ya nchi za bara hili, kupanua soko la biashara na fedha, kugeuza Asia kuwa mshirika mwenye uwezo wa kushirikiana na nchi nyingine za dunia na kunyanyua nafasi ya Asia kwa ajili ya kuiwezesha kuwa athirifu katika milingano ya ya kimataifa. Sekretarieti na makao makuu yake kwa sasa yako Kuwait. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilijiunga na jumuiya hii mwaka 2004, ambapo imekuwa mwenyekiti wake wa mzunguko tangu mwaka jana baada ya kuchukua nafasi hiyo kutoka kwa Bahrain. Mipango na vikao kadhaa vimeandaliwa na Iran katika kipindi cha uenyekiti wake kwa lengo la kuimarisha shughuli za jumuiya hiyo ikiwa ni pamoja na kuandaa kikao cha mawaziri wa mambo ya nje mjini Tehran, kikoa cha wakuu wa vyumba vya biashara mkoani Isfahan na kongamano la mawaziri wa utalii mkoani Yazd.

Mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia mjini Tehran

Kufanyika mjini Tehran kikao cha 19 cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia mjini Tehran kwa kuhudhuriwa na idadi kubwa ya mawaziri na maafisa wakuu wa nchi za Asia baada ya Iran kumpoteza Shahidi Rais Raisi na waziri wake wa  mambo ya nje na katika kukaribia kufanyika uchaguzi wa 14 wa rais, kuna umuhimu maradufu kwa Iran. Kufanyika mkutano huu mjini Tehran pia kuna umuhimu wa aina mbili. Kwanza kabisa; uenyekiti wa Iran katika Jumuiya ya Ushirikiano wa Asia kunaashiria kushindwa kwingine kwa wapangaji wa njama ya kutengwa Iran kieneo na kimataifa. Pili, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa ikisisitiza juu ya kuimarishwa ushirikiano wa kiuchumi katika fremu ya jumuiya hiyo kwa lengo la kunufaika na tajiriba za kiviwanda, kiuchumi na kiufundi za nchi wanachama.

Ushirikiano katika nyanja za mawasiliano, sayansi, teknolojia na uvumbuzi, elimu na maendeleo ya rasilimali watu, usalama wa chakula, nishati na maji, utamaduni na utalii, maendeleo endelevu na jumuishi na kuchunguza njia za kuwasaidia watu wa Palestina ni ajenda muhimu ya mkutano wa Tehran. Wazo la kuanzishwa Jumuiya ya Mazungumzo ya Ushirikiano wa Asia lilipendekezwa kwa mara ya kwanza na Waziri Mkuu wa Thailand na kujadiliwa katika Mkutano wa 34 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa ASEAN mnamo 2001. Kikao cha juu kabisa cha jumuiya hii ni mkutano wa Mawaziri wa Mambo ya Nje, ambao hufanyika mara mbili kwa mwaka, wa kwanza ukiwa ni ule unaofanyika kando ya mkutano wa mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York na wa pili huandaliwa na nchi mwenyekiti katika mwaka huo.

Mkutano wa kwanza wa mawaziri wa mambo ya nje wa jumuiaya hii ulifanyika nchini Thailand mnamo 2002 kwa kuhudhuriwa na wawakilishi wa nchi 18 wanachama, ambapo mawaziri wa mambo ya nje wa nchi zilizoshiriki mkutano huo waliunga mkono kuimarishwa na kuendelezwa shughuli za jumuiya. Takriban miaka minne baada ya kuanzishwa kwake, idadi ya nchi wanachama iliongezeka kutoka nchi 18 hadi 33. Kwa sasa jumuiya hii ina wanachama 35 ambao ni Iran, Thailand, Indonesia, Malaysia, Philippines, Brunei, Singapore, Cambodia, Vietnam, Myanmar, Laos, Nepal, Russia, Uturuki, Japan, China, Mongolia, Korea Kusini, India, Afghanistan, Pakistan, Bangladesh, Sri Lanka, Bhutan, Kuwait , Bahrain, Saudi Arabia, Qatar, Falme za Kiarabu, Oman, Palestine, Kazakhstan, Uzbekistan, Kyrgyzstan na Tajikistan. Jumuiya hii ya Asia ambayo ina nusu ya idadi ya watu wote duniani, ina karibu asilimia 30 ya pato jumla la kitaifa duniani.

Tags