Aug 03, 2024 10:53 UTC
  • Iran yaishukuru Algeria kwa kuiunga mkono katika mkutano wa Baraza la Usalama

Ali Bagheri, Kaimu Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran amefanya mazungumzo ya simu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Ahmed Ataf kuhusiana na matokeo ya kitendo cha kigaidi cha utawala wa Kizayuni cha kumuua shahidi Ismail Haniyeh, Mkuu wa Ofisi ya Kisiasa ya harakati ya Hamas na kuishukuru Algiers kwa uungaji mkono wake kwa kadhia ya Palestina.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Kaimu wa Waziri wa Mambo ya Nje ya Iran, mbali na kumshukuru Spika wa Bunge la Algeria kwa kuhudhurisha sherehe za kuapishwa Rais wa awamu ya 14 wa Iran amesisitiza kuwa, utawala wa Kizayuni umevuka mstari mwekundu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa kumuua shahidi Ismail Haniyeh ndani ya ardhi ya Iran.

Vile vile ameishukuru Algeria kwa uungaji mkono wake kwa kadhia ya Iran katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kilichojadili jinai ya utawala wa Kizayuni ya kumuuua shahidi Ismail Haniyeh, na pia amesisitizia wajibu wa kufanyika kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu OIC, katika ngazi ya mawaziri wa mambo ya nje ili kuchunguza na kuchukua maamuzi juu ya jinai hiyo ya Israel.

Katika mazungumzo hayo ya simu, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria kwa mara nyingine tena ameunga mkono hatua ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ya kutaka kufanya kikao cha dharura cha Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu kwa ajili ya kukabiliana na vitendo vya kigaidi vya utawala wa Kizayuni.

Vile vile amesisitizia msimamo wa serikali na wananchi wa Algeria wa kulaani vikali jinai ya utawala wa Kizayuni katika mauaji ya Ismail Haniyeh na kusema kuwa jinai hiyo imekanyaga mamlaka ya kujitawala taifa la Iran.