Iran: Mafanikio yetu katika uga wa teknolojia ni pigo kwa maadui
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa, hatua ya satelaiti ya utafiti ya Iran iliyopewa jina la "Chamran-1" kurushwa katika anga za mbali kwa mafanikio ni pigo kwa maadui wanaoliwekea taifa hili vikwazo visivyo na mantiki.
Nasser Kana'ni amesema katika ujumbe alioutuma kwenye akaunti yake ya mtandao wa kijamii wa X kwamba, kwa kurushwa kwa mafanikio satelaiti ya utafiti ya Chamran-1 kwa kutumia chombo cha kubeba satelaiti cha Qaem 100 na kuwekwa kwenye mzunguko wa kilomita 550 wa dunia ni baraka kwa Wairani wote maazizi, wanasayansi wa Iran, na wasomi haswa wale waliohusika katika mafanikio haya ya kujivunia.
Amewahutubu Wamagharibi kwa kuwaambia, "Waweka vikwazo wasio na mantiki kwa mara nyingine tena wamewekewa wazi jibu la vitendo vyao visivyo na mantiki."
Kan'ani amebainisha kuwa, Iran ni mdau mwenye mantiki, mwenye nguvu na mwenye kujenga na kuongeza kuwa, ni bora kwa Wamagharibi kutathmini upya mienendo ya matamshi yao.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Fars, satalaiti hiyo ya Chamran-1 imeundwa na Shirika la Kielektroniki la Anga za Mbali (SAIRAN) kwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Anga na mashirika mengine ya kiteknolojia katika sekta binafsi nchini Iran.
Satelaiti hiyo yenye uzito wa kilo 60 ni ya utafiti kuhusu shughuli za anga za mbali na tayari imeshaanza kutuma taarifa zake. Roketi ya Qaim 100 ambayo imebeba satelaiti hiyo kwa mafanikio na kuifikisha katika mzingo wa dunia imeundwa na wataalamu wa Kikosi cha Wanaanga cha Jeshi la Iran la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC).