Sep 16, 2024 02:53 UTC
  • Qalibaf: Madai ya uwongo ya nchi za Magharibi yanakwamisha mazungumzo yenye tija

Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) amesema kuwa hakutakuwepo mazungumzo yoyote yenye tija maadamu nchi za Ulaya na nyingine za Magharibi zinataka kuandaa mazingira kwa ajili ya mashinikizo zaidi kwa kutoa madai ya uwongo.

Mohammed Baqer Qalibaf, Spika wa Bunge la Iran alisema jana katika kikao cha bunge hilo kuwa tuhuma zisizo na msingi za nchi za Magharibi hususan Troika ya Ulaya kuhusu Iran zinaonyesha uungaji mkono wao wa kibubusa kwa utawala wa Kizayuni na kwamba tuhuma hizo zinatoa ujumbe kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kutokuwa na imani na nchi hizo. 

Qalibaf amesisitiza kuwa, hatua ya nchi za Ulaya ya kukariri madai ya uwongo kwa kutegemea misimamo ya utawala ambao unajulikana kwa uwongo yaani utawala wa Israel haiwiani na matakwa ya kidiplomasia na kufanya mazungumzo. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani kwa  niaba ya Troika ya Ulaya Jumanne alasiri wiki iliyopita ilitoa taarifa na kutangaza vikwazo vipya kwa sekta ya usafiri wa anga ya Iran. 

EU na vikwazo vipya dhidi ya sekta ya usafiri wa anga ya Iran 

Katika kikao hicho cha bunge, Spika wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu ya Iran (Bunge) aliashiria pia suala la umoja kati ya Waislamu ulimwenguni na akasema: Hivi leo Waislamu duniani wana sauti moja na wanakubaliana kuhusu kadhia ya Palestina.

 

Tags