Masomo tunayojifunza kutokana na kujitetea kutakatifu, miaka 36 baada ya kumalizika vita
Miaka 36 imepita tangu kumalizika vita vya miaka 8 ambavyo utawala wa Baath wa Iraq uliitwisha Iran, vita ambavyo vimeacha nyuma mafunzo na ibra nyingi zilizo wazi, 4 kati ya hizo zikiwa muhimu zaidi.
Somo la kwanza la vita vitakatifu ni kwamba umoja hutatua matatizo mengi na kuandaa uwanja wa kumshinda adui. Licha ya utawala wa Baath wa Iraq kuungwa mkono na madola yote ya kikanda na kimataifa katika vita hivyo vya miaka 8, lakini mwishowe, haukuweza kuchukua hata inchi moja ya ardhi ya Iran. Kujitetea kutakatifu ni mojawapo ya maonyesho ya wazi zaidi ya umoja wa kitaifa ulioonyeshwa na wananchi shupavu wa Iran bila kujali dini, madhehebu, makabila na rangi zao. Suala hili linaonyesha kwamba maslahi ya kitaifa ni mstari mwekundu na msingi wa pamoja kati ya matabaka yote ya kifikra, kikabila, kijamii na kisiasa nchini Iran, maslahi ambayo yanaweza kuchukuliwa kuwa mtaji muhimu katika kuimarisha mshikamano kwenye mfumo wa maamuzi ya kitaifa.
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema jana Jumamosi asubuhi katika gwaride la vikosi vya jeshi kwa mnasaba wa Wiki ya Kujitetea Kutakatifu kwamba: "Ni umoja wa vikosi vya kijeshi na wananchi wote wapendwa wa Iran ya Kiislamu ndio ulioweza kuzima hujuma za kikatili za nchi za kikoloni kwa lengo la kuiangamiza Iran na Mapinduzi ya Kiislamu, na hivyo kuzifanya zikate tamaa."
Somo la pili muhimu la kujitetea kutakatifu ni kwamba ili kulinda ardhi yote ya nchi, ni dharura kuimarisha nguvu za kijeshi kiasi kwamba adui asithubutu kushambulia nchi, na iwapo atafanya kitendo kama hicho, akabiliwe na jibu kali kwa namna ambayo kosa hilo litamfanya agharamike pakubwa. Hivyo, ni stratijia ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwamba haikubali hata kidogo matakwa ya adui ya kutaka kuzungumzia uwezo wake wa makombora, stratijia iliyojengeka juu ya msingi wa uhalisia wa mambo na ambayo inailazimu kufanya juhudi maradufu kwa ajili ya kuimarisha zaidi na zaidi uwezo wake huo makombora. Bila shaka sehemu muhimu ya usalama wa Iran inategemea nguvu zake za kijeshi.
Kuhusiana na hilo, Rais Masoud Pezeshkian pia amesema: "Kama majeshi haya yasingekuwa na nguvu na uwezo wa kutosha, leo Iran isingekuwa salama na nchi na wananchi wasingekuwa na usalama wala amani."
Somo la tatu muhimu la kujitetea kutakatifu ni kwamba hatupaswi kutegemea nchi za kigeni katika kujidhaminia usalama wa kuaminika na kujilinda dhidi ya maadui wa kigeni. Utawala wa Baath wa Iraq ulianza kuishambulia Iran kwa kutegemea madola ya kigeni, na kudhani kwamba ungeweza kuishinda Iran na kufikia lengo lake la kujitanua katika eneo kwa kuungwa mkono na madola hayo, lakini ulishindwa kutimiza lengo hilo.
Wakati huo huo, waungaji mkono wa Iraq katika miaka 8 ya vita vya kulazimishwa, baada ya nchi hiyo kuishambulia Kuwait, waliamua kuishambulia Iraq na kuiwekea vikwazo vizito. Walianzisha vita dhidi ya nchi hiyo mwaka 2003 na hatimaye kuung'oa madarakani utawala wa Baath. Hatima ya utawala wa Baath nchini Iraq ni ushahidi tosha kwamba kuamini na kuyategemea madola ya kigeni hakuipelekei nchi yoyote kuwa na nguvu, hususan nchi za Kiislamu.
Somo la nne muhimu la kujitetea kutakatifu ni kwamba ushirikiano na uhusiano mkubwa kati ya raia na serikali unaweza kuwa chanzo cha mageuzi muhimu nchini. Wakati huo huo, mgawanyiko kati ya raia na serikali kuna matokeo mengi mabaya. Moja ya sababu za ushindi katika vita vya miaka 8 ni uhusiano mkubwa uliokuwepo kati ya raia na serikali, na kwa maneno mengine, mtaji mkubwa wa kijamii ulioletwa na Mapinduzi ya Kiislamu. Miaka 36 baada ya kumalizika vita vya miaka 8 vya Iraq dhidi ya Iran, suala hili muhimu, yaani hitajio la kulindwa na kuimarishwa mtaji huu muhimu wa kijamii, linapaswa kupewa kipaumbele na viongozi wote wa serikali.