Ombi la Iran kwa BRICS
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i116876-ombi_la_iran_kwa_brics
Kuacha kutumia sarafu ya dola, kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja vya nchi za Magharibi, kuwa na sekretarieti ndogo na ya haraka na kufanyika vikao vya BRICS katika nchi wanachama kwa mujibu wa hali ya kijiografia, ni matakwa manne yaliyowasilishwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa kundi la BRICS pambizoni mwa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York.
(last modified 2024-09-28T08:02:12+00:00 )
Sep 28, 2024 08:02 UTC
  • Ombi la Iran kwa BRICS

Kuacha kutumia sarafu ya dola, kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja vya nchi za Magharibi, kuwa na sekretarieti ndogo na ya haraka na kufanyika vikao vya BRICS katika nchi wanachama kwa mujibu wa hali ya kijiografia, ni matakwa manne yaliyowasilishwa na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika kikao cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa kundi la BRICS pambizoni mwa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa huko New York.

Sayyid Abbas Araqchi Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika kikao hicho kuhusu kutumiwa sarafu za kidijitali, kuzindua majukwaa ya pamoja ya benki na kutumiana jumbe za pamoja, kuanzisha miundo mbinu mipya ya kifedha na kibenki katika fremu ya BRICS n.k. Ukweli wa mambo ni kuwa nchi zinazopigania kuwa huru na zile zilizo huru duniani zimedhamiria kujitoa katika udhibiti wa ukoloni na matumizi ya sarafu za nchi za Magharibi khusuan sarafu ya dola.

BRICS kuachana na matumizi ya dola 

Kufikiwa lengo hili tajwa ni takwa kuu la nchi za ulimwengu wa  kusini,  na ni nguzo ya kukabiliana na ukoloni wa Magharibi na matakwa yao. Mbali na hili, nchi wanachama wa BRICS zinataka kuchukuliwa hatua za dhati na za haraka ili kukabiliana na vikwazo vya upande mmoja vya nchi za Magharibi hasa Marekani ambavyo vimeziathiri aghalabu ya nchi hizo.

Sayyid Abbas Araqchi amesema kuwa moja ya vigezo vilivyotajwa katika nyaraka za BRICS ni kupinga na kutofungamana na vikwazo vya upande mmoja na haramu vya nchi za Magharibi hususan Marekani. Kwa msingi huo, Tehran inaona kuwa kuna umuhimu na haja ya kuwepo fikra na hatua za pamoja ili kutekeleza mifumo mbalimbali ya kukabiliana kwa pamoja na vikwazo ndani ya BRICS; na kundi hili litashindwa kukidhi matarajio ya wanachama wake katika kutafuta kutatua matatizo ya kifedha yanayowakabili iwapo hakutakuwa na kasi nzuri ya  utendaji katika masuala ya fedha, benki, biashara, uwekezaji, usafirishaji, teknolojia na uvumbuzi.

Nchi wanachama wa BRICS

Wakati huo huo kupanuliwa shughuli, matukio na programu za BRICS katika nguzo tatu za kisiasa-kiusalama, kiuchumi-kifedha na kiutamaduni na kiraia sambamba na kuongezeka idadi ya nchi wanachama kunailazimu BRICS kuwa na sekretarieti ndogo na inayofanya kazi kwa kasi inayohitajika hasa katika siku zijazo, na hivyo kupanuka na kuwa chombo athirifu zaidi kufuatia kuongezeka idadi ya nchi washirika katika kundi hilo. 

Kwa kuzingatia udharura huu, inapasa kwenda sambamba na kupanua shughuli zake katika kuaasisi mifumo ya kitaasisi kama vile kubuni sekretariati ndogo. Wakati huo huo, kuwa na programu 258 na kushuhudiwa matukio mbalimbali katika kipindi cha mwaka mmoja ndani ya kundi la BRICS ni jambo nadra kuwahi kushuhudiwa kwa makundi na taasisi za kimataifa. Kwa mtazamo wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ni vigumu kutekelezwa programu zote hizo katika nchi moja tu ambayo ni mwenyekiti wa kiduru wa kundi hilo. Kwa msingi huo, Tehran imependekeza kwamba baadhi ya matukio na programu za BRICS zinapasa kusambazwa kijiografia miongoni mwa wanachama. 

Ala kulli haal, kuasisiwa kundi la  BRICS kumeibua fursa nyingi za matumaini kwa ulimwengu wa kusini ili kujinasua katika udhibiti wa kifedha wa nchi za Magharibi kupitia kuimarisha ushirikiano kati yao. Kutambuliwa suala hili kunategemea ugawanaji wa majukumu miongoni mwa wanachama, kuimarishwa mamlaka na uwezo wa taasisi na kuandaliwa mazingira athirifu mkabala wa matumizi ya sarafu za kitaifa na za ndani; na hili linapasa kujumuisha hali za nchi wanachama wote wa BRICS.