Rais Pezeshkian: Iran itatoa jibu kali zaidi iwapo Israel itafanya 'kosa'
(last modified Thu, 03 Oct 2024 12:56:43 GMT )
Oct 03, 2024 12:56 UTC
  • Rais Pezeshkian: Iran itatoa jibu kali zaidi iwapo Israel itafanya 'kosa'

Rais Masoud Pezeshkian wa Iran amesema Iran bila ya shaka itatoa jibu lenye "nguvu na la kukandamiza zaidi" kwa utawala haramu wa Israel ukiwa utafanya hata kosa "dogo" tu la kujaribu kujibu shambulizi kulipiza kisasi lililofanywa Jumanne usiku na Iran kwa kuyatwanga kwa makombora maeneo nyeti ya kijeshi na kiusalama ya utawala wa Kizayuni.

Pezeshkian, ambaye yuko katika ziara ya siku mbili nchini Qatar, alitoa kauli hiyo jana Jumatano wakati alipokutana na ujumbe wa ngazi za juu wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas. Mkutano huo ulikuja siku moja baada ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kutekeleza operesheni ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel iliyopewa jina la Operesheni ya Ahadi ya Kweli II.

Amezikosoa nchi za Magharibi kwa kutoa ahadi tupu na kusema kuwa ziliitaka Iran kujizuia na kujiepusha kutoa jibu la mauaji yaliyofanywa na utawala wa Israel Julai Mosi dhidi ya Ismail Haniyeh mkuu wa ofisi ya kisiasa ya Hamas mjini Tehran na mkabala wa hilo ilikuwa ni kuanzishwa usitishaji vita huko Gaza na kukomeshwa mauaji ya kimbari dhidi ya Wapalestina wa ukanda huo.

Amesema lakini ahadi hizo hazikutekelezwa na jinai za utawala wa Kizayuni zimeendelea ndio maana Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetoa jibu la uhakika.

Rais wa Iran amelaani ukatili unaofanywa na Israel huko Gaza na Lebanon, na kukemea Marekani na nchi za Magharibi kwa kufuata mbinu za kinafiki, akisema zinaiunga mkono Israel huku zikidai kutetea demokrasia na haki za binadamu.

Aidha Rais wa Iran amesisitiza ulazima wa kustawishwa mshikamano baina ya mataifa ya Kiislamu na kusisitiza kuwa, kukosekana umoja huo kumeupa moyo utawala wa Israel wa kutekeleza jinai zaidi dhidi ya wananchi madhlumu wa Palestina na Lebanon.