Sisitizo la kustawisha uhusiano kati ya Iran na India
(last modified Thu, 24 Oct 2024 09:44:53 GMT )
Oct 24, 2024 09:44 UTC
  • Sisitizo la kustawisha uhusiano kati ya Iran na India

Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi wamejadili njia za kuendeleza uhusiano kati ya Tehran na New Delhi pambizoni mwa mkutano wa 16 wa wakuu wa nchi za BRICS huko Kazan, Russia.

Katika mkutano huo, Pezeshkian ameutaja ujumbe na jitihada za Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuwa ni kueneza amani na urafiki duniani. Mbali na mkutano wa wakuu wa kundi la BRICS kuwa muhimu katika kuathiri matukio ya dunia; kushiriki wakuu wa nchi mbalimbali duniani katika tukio hilo muhimu la kimataifa kunawaandalia fursa nzuri  ya kujadili masuala muhimu ya pande mbili katika mikutano ya nchi hizo mbili na wakati huo huo kufanya jitihada za kuimarisha mahusiano kati ya pande mbili.

Kwa msingi huo, Waziri Mkuu wa India baada ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, ametuma ujumbe katika mtandao wa kijamii wa X kwa lugha ya Kifarsi kwamba: 'Katika mazungumzo yake na Rais wa Iran wamechunguza suala la uhusiano kamili kati ya nchi mbili.'

Narendra Modi, Waziri Mkuu wa India 

Kwa hiyo, mbali na masuala muhimu zaidi ya pande mbili, matukio ya kikanda pia yamejadiliwa katika mkutano kati ya viongozi wa Iran na India. 

Uhusiano wa Iran na India siku zote umekuwa ukistawi kwa kutilia maani masuala ya pamoja kiutamaduni, kiustaarabu na hata kilugha ambapo jitihada za nchi za Magharibi za kuathiri vibaya uhusiano huo zimegonga mwamba. 

Mbali na uhusiano wa kibiashara, Iran na India zina uwezo mkubwa wa uwekezaji, mojawapo ikiwa ni bandari ya kimataifa ya Chabahar katika Bahari ya Oman. 

Bandari ya Chabahar, ambayo India inahusika katika baadhi ya awamu zake za ujenzi inatoa fursa kubwa kwa India ili kufikia masoko muhimu ya kikanda, ikiwa ni pamoja na Afghanistan, Asia ya Kati na Kafkazi ya Kusini. 

Kwa kuzingatia kuongezeka pakubwa umuhimu wa kupatikana njia za mawasiliano za gharama ya chini na salama; njia za mawasiliano za Iran sawa kabisa na njia nne za kimataifa zimesifiwa na duru za kimataifa hasa nchi zile zinazoongoza kwa kusafirisha bidhaa nje ya nchi. 

Kwa msingi huo, inatazamiwa kuwa India itaimarisha nafasi yake ya mawasiliano ya usafiri na nchi za  kanda hii kwa kutekeleza ahadi zake katika bandari ya Chabahar.

Katika sekta za nishati, viwanda, kilimo na teknolojia pia Iran na India zina uwezo na suhula nyingi kwa ajili yakustawisha uhusiano kati yazo; ambapo mazungumzo kati ya wakuu wa nchi mbili hizo yataweka wazi suala hili.  

Wakati huo huo, Iran na India sio tu zina uwezo unaohitajika wa kuchochea maendeleo ya kikanda na kimataifa katika fremu ya taasisi za kikanda kama vile BRICS na Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) bali, kutokana na kuwepo masuala mengi yanayofanana katika misimamo na mitazamo ya kikanda na kimataifa, Tehran na New Delhi zinaweza kuwa na taathira katika masuala ya kikanda na kimataifa kupitia mashauriano na uratibu baina yazo. 

Kuhusiana na suala hilo, Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Narendra Modi Waziri Mkuu wa India katika mazungumzo hayo katika mji wa Kazan nchini Russia wamechunguza kadhia muhimu zaidi za pande mbili na njia za kuimarisha uhusiano wa muda mrefu na wakati huo huo kuchunguza pia matukio ya kikanda na kutilia mkazo udharura wa kusitishwa mapigano katika eneo la Asia Magharibi na kujiepusha na uchukuaji wa maamuzi na misimamo ya undumakuwili kuhusu haki za binadamu. 

Rais Masoud Pezeshkian katika mazungumzo na Narendra Modi huko Kazan, Russia

Hata kama India ina uhusiano mzuri na Magharibi, lakini wakati mwingine hukabiliwa na hasira za nchi za Magharibi pale inapotekeleza sera huru mkabala wa mahusiano ya kikanda na kimataifa. Kwa msingi huo, inaonekana kuwa ni muhimu kwa nchi kama Iran na India kufungamana na mstari wa kujitawala na kuwa huru katika sera zao ili kuzidisha  mchango wao athirifu katika matukio ya kikanda na kimataifa ikiwa ni pamoja na vita vya umwagaji damu vya Gaza na Lebanon kufuatia kubadilika hali ya mambo kimataifa na kuundwa taasisi zenye nguvu kama BRICS.