Iran yasema iko tayari kujibu uchokozi na uvamizi wa Israel
(last modified Sat, 26 Oct 2024 10:02:49 GMT )
Oct 26, 2024 10:02 UTC
  • Iran yasema iko tayari kujibu uchokozi na uvamizi wa Israel

Duru za kuaminiki zimeliambia shirika la habari la Tasnim kwamba, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ipo tayari na imejiandaa kujibu chokochoko za utawala wa Kizayuni wa Israel.

Tasnim imeinukuu duru hiyo ikieleza kuwa: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ina haki ya kutoa jibu mkabala wa hatua yoyote ya kichokozi dhidi yake.

Wakati huo huo, Fatemeh Mohajerani, Msemaji wa serikali ya Iran amesema leo Jumamosi kwamba, uharibifu wa mashambulizi ya usiku wa kuamkia leo ya Israel dhidi ya Iran ni "kiduchu" na kwamba hali ya nchi ni "ya kawaida" na shwari.

Akizungumzia kuenea kwa picha za uongo na ripoti ambazo hazijathibitishwa, Mohajerani amewataka wananchi wa Iran kuwa watulivu na wajiepushe na kuamini uvumi, akiwahimiza kutegemea tu vyombo rasmi vya habari na taarifa kutoka kwa vikosi vya ulinzi wa anga vya Iran kwa na maelezo sahihi.

Fatemeh Mohajerani, Msemaji wa serikali ya Iran

Mohajerani pia amelipongeza jeshi la anga la Iran kwa hatua yao ya kulinda kwa nguvu maeneo ya kijeshi dhidi ya mashambulio ya Israeli akisisitiza kuwa, hatua hiyo imehuisha fahari ya kitaifa ya Wairani.

Kabla ya hapo, Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu la Iran (IRGC) lilikuwa limesisitiza kuwa, vikosi vya ulinzi vya nchi hii vimejiandaa kikamilifu kujibu tishio lolote dhidi ya nchi hii kufuatia kupamba moto mivutano katika eneo.

 

Tags